Karagwe FM
Karagwe FM
10 May 2025, 11:14 am

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoa wa Kagera imeendelea kufuatilia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za serikali na kubaini baadhi ya changamoto ikiwa ni pamoja na uwepo wa kundi la watu wanaofanya utapeli kwa wananchi wanaodaiwa kutozwa fedha ili kuwezesha miradi kutekelezwa kwenye maeneo yao
Theophilida Felician, Bukoba.
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU mkoa wa Kagera imewasaidia wananchi 9 wa kijiji cha Bulembo kata ya Ibuga wilayani Muleba kupata fedha zao shilingi 2,300,000/= waliyokuwa wametapeliwa na watu wawili kwa madai ya kuwaunganishia huduma ya umeme.
Akitoa kauli hiyo kwa wandishi wa habari Kaimu mkuu wa TAKUKURU wa Kagera Hajinas Onesphory tarehe 9 Mei 2025 katika makao makuu ya taasisi hiyo manispaa ya Bukoba amesema watu hao ambao ni Patrick Muchunguzi na Revocatus Masanja waliwafikia wananchi hao wakiwaongopea kuwaunganishia umeme jambo ambalo halikuwa la kweli kwani kijiji hicho hakikuwa kwenye mpango wa huduma hiyo, hivyo watu hao waliitumia lugha ya kuwalaghai na kufanikiwa kujikusanyia fedha kinyume cha sheria.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU mkoa wa Kagera imebaini kutokuwepo vigae vilivyohusishwa na zaidi ya shilingi milioni 50 zinazoripotiwa kutokuwasilishwa na mzabuni kwenye mradi wakati nyaraka zote zikionesha kwamba vifaa hivyo vimenunuliwa na kupokelewa.
Kutokana na juhudi za TAKUKURU hadi sasa vigae hivyo vimefikishwa kwenye mradi wa Hospitali ya wilaya ya Missenyi
Hajinas amewasihi wananchi kuendelea kutoa taarifa za viashiria vya rushwa ili kuitokomeza ipasavyo hususani kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Rais.