Karagwe FM

Wazazi wa watoto ambao hawajaripoti shule kusakwa Karagwe

17 February 2025, 7:44 am

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mshabaiguru wilaya ya Karagwe wakiwa katika mkutano wa kijiji.Picha na Jovinus Ezekiel

Na: Jovinus Ezekiel

Uongozi wa kata ya Kihanga wilayani Karagwe mkoani Kagera umeazimia kuanza kutekeleza mpango wa kuwasaka wazazi na walezi ambao watoto wao hawajaripoti shuleni tangu shule zifunguliwe katika kipindi cha mwezi Januari mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mshabaiguru kata ya Kihanga wilayani Karagwe Februari 14.2025 ukiwa na lengo uongozi kupitia kwa diwani wa kata hiyo Stephen Rwamuhangi Mugasha kusikiliza kero za wananchi, kupitia katika mkutano huo afisa mtendaji wa kata ya Kihanga William Pius amesikitishwa na idadi ya baadhi ya watoto ambao hawajaripoti shuleni na kusema kuwa kwa sasa uongozi wa kata ya Kihanga utahakikisha unaanza msako mara moja wa kuwapata wazazi na walezi ambao watoto wao hawajaripoti shuleni.

WEO Kihanga wilaya ya karagwe William Pius.Picha na Jovinus Ezekiel

Amesema kuwa mpaka sasa inasikitisha sana kuona wazazi na walezi hawajawapeleka watoto wao waliofaulu  kujiunga na kidato cha kwanza katika kata hiyo hali inayoweza kuongeza idadi kubwa ya watoto ambao hawana elimu.

Sauti ya Weo Kihanga William Pius

Diwani wa kata ya Kihanga Stephen Rwamuhangi Mugasha katika suala hilo ameunga mkono suala la wazazi na walezi ambao watoto wao hawajaripoti shuleni kwani serikali ya awamu ya sita imejitahidi kuboresha miundo mbinu ya elimu kwa lengo la wanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari kunufaika na elimu.

Sauti ya diwani wa kata Kihanga wilaya Karagwe Stephen Rwamuhangi Mugasha

Nao baadhi ya wananchi wa kata hiyo Shabibu Abdul na Salima Ramadhan wamesema kuwa elimu ni msingi wa maisha hivyo suala la wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shuleni ni muhimu kuliko kuendelea kuwafanya wajikite na shughuli za kilimo na ufugaji.

Diwani wa kata ya Kihanga Stephen Rwamuhangi Mugasha.Picha na Jovinus Ezekiel