Karagwe FM

CHADEMA Bukoba mjini walionya jeshi la polisi kuelekea uchaguzi mkuu 2025

9 February 2025, 6:09 pm

Mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA jimbo la Bukoba mjini Chifu Karumuna. Picha na Theophilida Felician

Chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA jimbo la Bukoba mjini kimeendelea kulalamikia mwenendo wa siasa hapa nchini na mara hii wakilionya jeshi la polisi kutofanya upendeleo kwenye uchaguzi mkuu ujao

Na Theophilida Felician, Bukoba

Chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema Bukoba mjini mkoani Kagera kimelitahadharisha Jeshi la polisi jimboni humo kikilitaka kutoshiriki hujuma za uchaguzi mkuu dhidi yao kama ilivyozoeleka chaguzi zilizopita ukiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024.

Akitoa tahadhari hiyo bila kupepesa macho kwenye mkutano wa hadhara wa chama kata ya Kashai mwenyekiti wa chama jimbo Chifu Karumuna amesema jeshi la polisi kutumika kwenye hujuma za uchaguzi imekuwa nichangamoto kwao kwani husababisha wao kunyanyasika hatimaye kufanya vibaya kwenye matokeo ya kura.

Chifu amefafanua kuwa kupitia nguvu ya vyombo vya dola likiwepo jeshi la polisi wamekuwa wakiwekwa madarakani viongozi ambao sio chaguo la wananchi kutoka chama cha mapinduzi CCM kama viongozi ambao ni wenyeviti na wajumbe waliopo sasa jambo linaloleta sintofahamu kwa wananchi.

Sauti ya mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA jimbo la Bukoba mjini Chifu Karumuna
Baadhi ya wananchi wa Kashai wakifuatilia hotuba ya mwenyekiti. Picha na Theophilida Felician

Kwa upande wake mwenyekiti wa baraza la wanawake jimbo BAWACHA Editha Bashanzi naye Katibu wa jimbo Sosthenes Andrea wameunga mkono kauli ya mwenyekiti Karumuna kutokukubali kuona uchaguzi ukihujumiwa na badala yake watapambana kwa hali na mali na jeshi hilo ili haki itendeke kwa vyama vyote.

Sauti ya mwenyekiti wa baraza la wanawake BAWACHA jimbo la Bukoba mjini Editha Bashanzi na katibu wa jimbo Sosthenes Andrea
Baadhi ya wananchi wa Kashai wakifuatilia hotuba ya mwenyekiti. Picha na Theophilida Felician