CHADEMA Bukoba DC kuzuia uchaguzi mahakamani
20 November 2024, 1:43 pm
Mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Bukoba vijijini bw. Deusdedith Rwekaza. Picha na Theophilida Felician
Wakati mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa ukiingia katika hatua ya kampeni, Chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA jimbo la Bukoba vijijini kimeeleza kuchukua hatua za kuzuia uchaguzi huo mahakamani kupinga TAMISEMI kuwaengua wagombea karibu wote wa chama hicho
Na Theophilida Felician.
Chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA jimbo la Bukoba Vijijini mkoani Kagera kimeapa kwenda mahakamani kwa ajili ya kutafuta haki ya kuwarejesha wagombea mia tano na sita (506) wa chama hicho walioenguliwa kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari katika ofisi za chama mjini Bukoba mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Bukoba vijijini bw. Deusdedith Rwekaza amesema kwamba taratibu zote zimekamilika na kilichobakia ni kwenda mahakamani kwa ajili ya kupinga mbinu zilizotumika kuvunja kanuni hadi kuwaengua wagombea wao ili waweze kurejeshwa hatimaye waweze kuendelea na uchaguzi kama walivyowateua.
Hata hivyo amewasihi wanachama kuwa watulivu kwa kipindi hiki wakati taratibu za kisheria zikiendelea huku akiahidi kuwa wao kama CHADEMA watahakikisha wanashiriki uchaguzi licha ya misukosuko hiyo.