Karagwe FM

Udumavu, watoto kukonda bado ni tatizo Kyerwa

13 November 2024, 12:44 pm

Afisa lishe wa halmashauri ya wilaya ya Kyerwa Irene Cleophace akifafanua jambo kwa wajumbe. Picha na Jovinus Ezekiel

Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa kama zilivyo halmashauri zingine mkoani Kagera inaendelea kutekeleza afua za lishe ili kupunguza udumavu na ukondefu kwa watoto

Na Jovinus Ezekiel

Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera imejipanga kuendelea kuboresha hatua za utaoji wa huduma za lishe katika jamii  kwa lengo la kufikia malengo ya kutokomeza udumavu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Akiwasilisha taarifa yake katika kikao cha robo ya kwanza cha kamati ya lishe katika halmashauri ya wilaya ya Kyerwa ambacho kimefanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo kwa kujumuisha wadau mbalimbali wa lishe wakiwemo baadhi ya viongozi wa dini Novemba 12. 2024, kupitia katika kikao hicho afisa lishe wa halmashauri ya wilaya ya Kyerwa Irene Cleophace amesema kuwa katika mpango wa miaka mitatu utakaodumu hadi mwaka 2028 ukilenga kutokomeza tatizo la udumavu katika halmashauri ya wilaya Kyerwa wakati mpango huo ukielekea kutekelezwa wao kama wataalam wamebaini kuwa katika jamii bado kuna watato ambao wanazaliwa na uzito pungufu hali inayoweza kuchangia hali hiyo.

Amesema kuwa katika dira ya kufanikisha mpango huo kama halmashauri ya wilaya ya Kyerwa kutokomeza udumavu ni kuendelea kuboresha hatua za utoaji wa huduma za lishe ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu.

Sauti ya afisa lishe wa halmashauri ya wilaya ya Kyerwa Irene Cleophace
Mwakilishi wa afisa elimu sekondari Bi Restuta Stephano (aliyesimama) akielezea hali ya lishe shuleni. Picha na Jovinus Ezekiel

Aidha kwa upande wake Restuta Stephano wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa lishe shuleni divisheni ya elimu sekondari kwa niaba ya afisa elimu sekondari wilaya ya Kyerwa amesema kuwa mpango wa wanafunzi kupata chakula shuleni unaendelea kutekelezwa ingawa wapo baadhi ya wanafunzi ambao wanakunywa uji bila kupata chakula.  

Sauti ya bi Restuta Stephano
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya lishe wilaya ya Kyerwa wakiwa kwenye kikao. Picha na Jovinus Ezekiel