DC Laiser adhamiria kuzuia matumizi ya mkaa Karagwe
13 November 2024, 11:24 am
Mkuu wa wilaya ya Karagwe Julius Kalanga Laiser ameshtushwa na ukataji mkubwa wa miti unaofanywa na wananchi kwa ajili ya kutengeneza mkaa hali inayotishia maisha kwa binadamu na wanyama kutokana na ukame siku za usoni
Na Edison Tumaini Anatory
Katika harakati za kulinda mazingira dhidi ya uharibifu mkuu wa wilaya ya Karagwe Julius Kalanga Laiza amelielekeza baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya hiyo pamoja na wataalam wake, kupitia sheria za mazingira ili kupata namna ya kuzuia kabisa matumizi ya mkaa.
Bwana Laiza amesema hayo wakati akilihutubia Baraza la madiwani la Halmashauri hiyo lililoketi Novemba 12 katika ukumbi wa Angaza mjini Kayanga.
Amesema kuwa, uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji wa miti kwa ajili ya uchomaji mkaa ni wa kiwango kikubwa akisema kuwa hakuna haja ya kusubiri kutokuchukua hatua ili kulinda mazingira.
Wakichangia mara baada ya uwasilishaji wa taarifa za madiwani kupitia kata zao wamesema kuwa madhara ya mabadiliko ya tabia nchi sasa ni dhahiri wilayani Karagwe kutokana na ukame unaoshuhudiwa huku baraza hilo likiazimia kuhakikisha wataalam wa kilimo wanawahimiza wakulima kulima mazao yanayostahimili ukame ili kujihami dhidi ya tishio la uhaba wa chakula.
Katika hatua nyingine madiwani hao wamefikia makubaliano ya kwamba wazazi wenye wanafunzi wanaosoma shule kuhakikisha wanapeleka mapema chakula cha wanafunzi shuleni kabla ya mwezi Januari, 2025 ili kuepuka gharama kubwa na wakati mwingine kukosekana kwa chakula cha kuwalisha wanafunzi shuleni siku za usoni.