Muleba Stars wachapwa 5-1 na BMC ya Bukoba kombe la Samia Kagera
9 November 2024, 10:17 pm
Burudani ya mpira wa miguu imeanza mjini Bukoba mkoani Kagera kupitia ligi ya Samia Kagera inayolenga kuwahamsisha vijana wa mkoa huu kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024
Theophilida Felician.
Pazia la mashindano ya Samia Kagera Cup 2024 limefunguliwa rasimikwa kuzikutanisha timu kutoka halmashauri za Muleba na Bukoba Manispaa ambapo katika mchezo huo wa ufunguzi timu ya halmashauri ya manispaa ya Bukoba (BMC) imeibuka na ushindi wa goli 5 dhidi ya goli 1 la timu ya Muleba stars ya halmashauri ya Muleba
Mashindano hayo ambayo yamezinduliwa tarehe 9 Novemba 2024 katika viwanja vya Kaitaba Manispaa ya Bukoba yamezikutanisha uso kwa uso timu hizo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali pamoja na mashabiki wa soka mkoani Kagera
Akizindua mashindano hayo mkuu wa mkoa Kagera Hajat Fatma Mwasa amesema kwamba mashindano ya Samia Kagera Cup yatakuwa endelevu kwa mkoa wa Kagera nia na madhumuni ikiwa ni kupanua wigo wa kuwaibua na kuwapata wachezaji bora hadi kuipata timu nyingine ya mkoa kama ilivyo kwa timu ya Kagera Sugar ambapo pia ametoa pongezi na shukrani kwa waandaaji wa ligi hiyo.
Kwa upande wake mwandaaji wa mashindano hayo ambaye ni mjumbe wa baraza kuu la umoja wa vijana kupitia UVCCM Taifa kutokea mkoa wa Kagera na mkurugenzi wa kampuni ya Clearing and Forwading (KPD) Leodgar Kachebonaho amesema mashindano hayo zaidi yamebeba ujumbe juu ya kuwahamasisha vijana na wananchi kwa ujumla kujitokeza na kushiriki ipasavyo zoezi muhimu la uchaguzi wa serikali za mitaa Tarehe 27 Novemba 2024.
Leodgaer amezitia moyo timu 8 kutoka halmashauri zote za Mkoa Kagera akiamini kuwa vijana wa timu hizo wako imara na zawadi nono zilizoandaliwa Sh Ml 10 kwa mshindi wa kwanza, Sh Ml 5 kwa mshindi wa pili na Sh Ml 3 kwa mshindi wa tatu zitapambaniwa vilivyo.
Hata hivyo mtanange wa Fainali ya ligi hiyo utachezwa mnamo Tarehe 23, Novemba 2024.