Samia Kagera Cup kutumika kuhamasisha uchaguzi
8 November 2024, 11:09 am
Mashindano ya mpira wa miguu “Samia Kagera Cup 2024” yanatarajia kuanza kutimua vumbi mkoani Kagera yakiwa na ujumbe wa elimu mahususi ya kuhamasisha wananchi kujitokeza na kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa 27 Novemba 2024.
Na Theophilida Felician
Mwanzilishi wa ligi maalumu ya mpira wa miguu maarufu kama “Samia Kagera Cup 2024” bw. Leodgar Leonard Kachebonaho amewaeleza waandishi wa habari akiwa ofisi ya mkuu wa mkoa manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kuwa mashindano hayo yatahusisha halmashauri zote 8 za mkoa wa Kagera kwa ajili ya kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na mambom mengine.
Amefafanua kuwa kamati husika iliwiwa kuyaita jina la Rais Samia kutokana na miradi mingi ya maendeleo iliyotekelezwa mkoani Kagera hivyo wakaona umuhimu wa mashindano hayo kuyapatia jina hilo la Samia Kagera Cup kama pongezi kwake.
Kachebonaho amezitaja zawadi kwa washindi akieleza kuwa mshindi wa kwanza atapokea shilingi milioni 10 na kwamba mashindano haya yatatumia wiki mbili hadi fainali itakayochezwa Novemba 23
Mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwasa awali amepongeza wazo la mashindano hayo na kusema kuwa wao kama serikali watakuwa na ligi hiyo bega kwa bega ili kuhakikisha inafanikiwa vyema ambapo hata hivyo katibu wa chama cha mpira wa miguu mkoa Kagera Al Amini Abdul amesema mashindano hayo yataanza tarehe 9 Novemba na kukamilika Tarehe 23 Novemba mwaka huu 2024 katika viwanja vya Kaitaba mjini Bukoba.