Mama auwawa na wasiojulikana akiwa kwake Karagwe
12 October 2024, 6:45 am
Wimbi la vitendo vya mauaji katika siku za hivi karibuni limehusishwa na kukithiri kwa matatizo ya afya ya akili, mmomonyoko wa maadili, uelewa duni wa namna ya kuishi, huku umasikini uliopitiliza nao ukitajwa kama moja ya sababu.
Na: Edson Tumain – Karagwe
Watu wanaosadikika kuwa majambazi wamemvamia Bi. Adorofina Kanyambo (46) mfanyabiashara mkazi wa kitongoji cha Bomani mjini Kayanga kisha kumuua.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, mwili wa marehemu umegundulika ndani Oktoba 11 majira ya asubuhi ukiwa umefungwa taulo shingoni huku kasiki iliyokuwa ikihifadhi fedha ikikutwa imefunguliwa.
Akiwa eneo la tukio ,Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Julius Kalanga Laizer ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya dola ili kuwabaini wahalifu waliohusika katika tukio hilo lakini pia akawaasa wafanyabishara kutohifadhi fedha ndani ya nyumba.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Longino Wilbard pamoja na Diwani wa Kata ya Kayanga Gelmanus Byabusha,wamelaani tukio hilo wakisisitiza umuhimu wa Ushirikiano kati ya wananchi na Vyombo vya dola kukomesha matukio ya mauaji na utekeji yanayozidi kushamiri Mjini Kayanga.
Ili kudhibiti wimbi la utekeji wa wafanyabiashara, Mwenyekiti wa TCCIA Wilayani Karagwe Livingistone Nestory amewakumbusha wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kuungana ili kujilinda na Majambazi.
Huku majonzi yakitawala katika eneo hilo, ndugu jamaa na marafiki wamelaani kitendo hicho walichokiita cha unyama.
Tukio la mauaji ya mama huyo Bi.Adorofina Kanyambo limetokea wakati mme wake Beatus Nyarugenda mfanyabiashara wa mitungi ya gesi na mmiliki wa kiwanda cha mikate kilichoko Mwisho wa lami mjini Kayanga akiwa safarini ambapo amelazimika kukatiza safari yake na kurejea nyumbani.