EWURA CCC Kagera yawataka wananchi kuwasilisha malalamiko
24 September 2024, 7:59 pm
Watumiaji wa huduma za nishati na maji mkoani Kagera wameendelea kunufaika na elimu ya namna ya kuwasilisha malalamiko yao kwenye baraza la ushauri la watumiaji wa huduma hizo EWURA CCC
Na Theophilida Felician
Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za maji na nishati EWURA CCC mkoa Kagera limetoa wito kwa wananchi likiwahimiza kujitokeza katika ofisi za baraza hilo ili kupata huduma kadhaa hususani elimu pamoja na kuwasilisha changamoto dhidi ya huduma za maji na nishati.
Ameyasema hayo Afisa msaidizi huduma kwa wateja na utawala baraza hilo Anadorice Komba wakati akitoa elimu kwa wananchi wa kata ya Rwamishenye Manispaa ya Bukoba na kusema kuwa wananchi iwapo watakuwa na mwitikio mzuri wa kuifikia ofisi hiyo watanufaika zaidi ikiwemo kupata taarifa sahihi na miongozo katika kuwasilisha malalamiko.
Amezitaja changamoto zinazowasilishwa na wananchi kwa EWURA CCC kuwa ni pamoja na wengi wao kufuatilia taarifa zao kwa watoa huduma bila mafanikio kutokana na mizunguko ambayo hukutana nayo kutoka kwa wahusika hivyo baraza hilo huchukuwa jukumu la kuwasadia wananchi kufuatilia kwa ukaribu kwa malengo ya kupata haki zao.
Hata hivyo ameongeza kuwa wakiwa Rwamishenye wananchi pia wamelalamika na kutoa maoni pamoja na ushauri kwa mamlaka husika za maji na nishati.
Moja ya malalamiko hayo ni Ankara kubwa za maji, kukatiwa huduma za maji bila taarifa, pamoja na tozo ya kodi ya majengo kupitia luku ya umeme.
Miongoni mwa wananchi hao yumo Jaziru Yassin ambaye ametoa ufafanuzi kuhusu kodi ya majengo kupitia luku ya umeme.
Anadorice amewahakikishia wananchi kuchukuwa malalamiko yao kwa watoa huduma ili yaweze kufanyiwa kazi.