‘Amani Kwanza’ Kagera wahofia video za kashfa dhidi ya Rais Samia
22 September 2024, 6:11 pm
Wananchi na makundi mbalimbali ya kutetea haki za binadamu mkoani Kagera wameitaka serikali kuchukua hatua thabiti dhidi ya viashiria vyote vyenye nia ya uvunjifu wa amani vilivyoanza kujitokeza kwa kasi hapa nchini.
Theophilida Felician
Katika kusherehekea siku ya amani duniani inayoashimishwa kila tarehe 21 septemba ya kila mwaka wito umetolewa kwa umma mkoani Kagera na nchi kwa ujumla kuungana pamoja na kuendelea kuitunza na kudumisha amani iliyodumu kwa muda mrefu huku serikali ikisisitizwa kuchukua hatua za haraka kivishughulikia na kuvidhibiti viashiria vya uvunjifu wa amani vinavyojitoleza kwa kasi maeneo mbalimbali nchini.
Yameelezwa hayo na wananchi pamoja na taasisi ya umoja wa Amani Kwanza wakati wakihojiwa na Redio Karagwe Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera ambapo awali mwenyekiti wa umoja wa Amani Kwanza Ndugu Maulid Rashidi Kambuga amesema kuwa kwa sasa kumekuwepo na masuala yenye kubeba viashiria vya uvunjifu wa amani kupitia nyanja mbalimbali akitolea mfano wa vidio chafu zenye jumbe za kichochezi zinazosambazwa mitandaoni na kuwafikia wananchi zikimtaja kiongozi mkuu wa nchi Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa ni muuaji jambo ambalo ni hatari sana kwa amani ya nchi.
Amesema kama jitihada za haraka hazitofanyika na kuyadhibiti haya kwa kuwabaini wahusika ili kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria yaweza tokea yasio mazuri tunakoelekea maana baadhi ya watu wasioitakia mema Tanzania wako macho hawajalala ndiyo maana chokochoko za hapa na pale zinaanza kupenyapenya ili kuhakikisha wanaididimiza amani iliyotukuka na kudumu kwa kipindi kirefu tangu kupata uhuru.
Kwa upande wao wananchi akiwemo Benard Pastory amesema kuwa ili amani kudumu ni vyema kila mmoja kuanzia ngazi ya chini hadi juu kulizingatia ipasavyo suala la maadili ambalo linaunganisha vitu vyote vyenye misingi imara kwa kila mtu na kwa kufanya hivyo suala la amani halitachezewa kama baadhi ya watu wanavyodhani ambapo pia Liston Kikanja ameeleza kwamba taifa letu lina amani tofauti na ilivyo kwa mataifa mengine yanayotaabika kwa sasa baada ya kukosekana kwa amani .
Hata hivyo Adolf Alane amevitaja baadhi ya vitu ambavyo kama havitotizamwa na kushughulikiwa vyaweza hatarisha amani ni pamoja na wimbi la rushwa katika siasa huku Hamza Idd akifafanua kuwa wananchi hawako tayari kuona amani inadondoshwa.
Kila mwaka ifikapo tarehe 21 Septemba ni siku ya amani duniani.