Karagwe FM

Katibu wa CHADEMA Kagera ahamia CCM akitaja uongo na ufisadi

11 August 2024, 9:50 pm

Aliyekuwa katibu wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA mkoa wa Kagera Dunstan Mutagahywa (mwenye vazi la CHADEMA kushoto). Picha na Theophilida Felician

Suala la viongozi wa kisiasa kuhama chama na kujiunga na chama kingine limekuwa jambo la kawaida hasa nyakati za chaguzi ndani ya vyama au kuelekea chaguzi muhimu za kitaifa

Na Theophilida Felician.

Aliyewahi kuwa katibu wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA mkoa Kagera Dunstan Mutagahywa ameachana na CHADEMA na kujiunga chama cha Mapinduzi CCM.

Akitangaza kupokelewa katibu huyo na makada wenzake hao 24 katibu wa itikadi na uenezi CCM Taifa Amosi Makalla Tarehe 10 Agost 2024 kwenye mkutano wa hadhara viwanja vya Mashujaa Mayunga Manispaa ya Bukoba amesema kuwa katibu Dunstan na wenzake baada ya kukiaga chama chao cha awali wamewapokea ili waungane nao safarini ndani ya CCM.

Baadhi ya wanachama wa CCM waliojitokeza kumsikiliza balozi Dkt Emanuel Nchimbi wakati wa ziara yake mjini Bukoba. Picha na Theophilida Felician

Makalla amesema wanaojiunga na CCM kutoka upande mwingine wanazitaja sababu mbalimbali ikiwemo ya kuvutiwa na kasi ya utendaji kazi wa serikali ya CCM katika ujenzi wa maendeleo ya nchi, demokrasia safi na mengineyo mengi ambapo amewakaribisha na wengine kwani milango iko wazi.

Naye Katibu Dunstan baada kupokelewa amepewa nafasi ya kusalimia na kuyataja baadhi ya mambo yaliyomkwaza hadi kuihama Chadema moja wapo amedai ni uongo uliotumika kuangamiza maisha ya watanzania bila kujua hususani wafuasi wao,ufisadi uliokithiri, pamoja na upigaji wa fedha za ruzuku zaidi ya Sh Bilioni 18 hadi kushindwa kufanya maendeleo ya chama kwani shughuli nyingi zikiwemo za ujenzi wa ofisi za chama wamekuwa wakitoa fedha mifukoni mwao kuwezesha shughuli hizo.

Aliyekuwa katibu wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA mkoa wa Kagera Dunstan Mutagahywa
Katibu mkuu wa CCM Balozi Dkt Emanuel Nchimbi (kulia> akimvalisha vazi la CCM bw. Mutagahywa mjini Bukoba. Picha na Theophilida Felician

Makada hao wamepokelewa na katibu mkuu wa CCM Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi naye amempongeza katibu huyo wa CHADEMA na wenzake kwa kuamua kurejea nyumbani.

Dkt Nchimbi amesema wataendelea kuwapokea kwa mikono miwili kutokana uimara wa CCM wanatarajia kuwapokea zaidi na zaidi.

Hata hivyo katibu huyo na viongozi alioambatana nao wameelezea shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na serikali chini ya Ilani ya CCM maeneo yote nchini hivyo amewaomba wananchi kuwaunga mkono kwa kuwachagua viongozi wanaotokana na CCM kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2025.

Sauti ya Katibu mkuu wa CCM Balozi Dkt Emanuel Nchimbi

Makada wapya wa CCM Wameahidiwa ushirikiano ndani ya CCM katika nyanja tofauti zaidi kuleta maendeleo kwa wananchi.