Karagwe FM

Waganga wa tiba asili Kagera walia na matapeli

7 August 2024, 9:44 pm

Katibu mkuu wa umoja waganga na wakunga wa tiba ya asili nchini (UWAWATA) bw. Lukasi Joseph Mlipu. Picha na Theophilida Felician

Huduma ya tiba asili mkoani Kagera imeendelea kukumbwa na changamoto ya kuingiliwa na watu wasio na ujuzi huo wakijivika mamlaka ya uganga na kuwatapeli wananchi kwa mwavuli wa uganga wa tiba asili

Na Theophilida Felician.

Waganga wa tiba asilia nchini wamehimizwa kuunga nguvu ya umoja jambo ambalo litawasadia kufikisha kilio kwa serikali kulingana na changamoto nyingi wanazokabiliana nazo katika taaluma yao.

Akitoa kauli hiyo katibu mkuu wa umoja waganga na wakunga wa tiba ya asili nchini (UWAWATA) Lukasi Joseph Mlipu wakati akizungumza na wanaumoja huo mkoa wa Kagera kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba amesema kwamba ni muda mrefu waganga nchini wanakumbwa na masaibu katika majukumu yao ya tiba.

Akizitaja baadhi yake ni pamoja na kasi ya kuchafuliwa kwa kuhusishwa na matukio ya kihalifu ambayo yamekuwa yakijitokeza kwenye jamii hususani ya mauaji kwa watu wenye ualbino.

Katibu mkuu wa umoja wa waganga na wakunga wa tiba ya asili nchini (UWAWATA) bw.Lukas Joseph Mlipu

Ameongeza kuwa kama serikali inagushwa na madhira ya waganga ishuke mamlaka za chini kwa nia ya wakuwasaidia ili nao wawe huru na waweze kushirikishwa mambo muhimu ya kijamii na hiyo itawaepushia zigo la kuwatwisha lawama ya uhalifu kitu ambacho siyo cha kweli.

Vile vile amesisita kwamba Ili kuyakabili hayo ni vyema pia waganga kuungana pamoja na kujisimamia na kuyasemea yale yote yanayowakumba hasahasa kashifa ya mauaji.

Hata hivyo amehitimisha akitoa wito akiwasihi waganga kujisajili ambao hawajapata leseni huku akiwakumbusha kujiunga na umoja huo ambao umekuwa msitali wa mbele katika kuzipambania kwa hali na mali haki za waganga hiyo ikiwa ni sambamba na kujitokeza Tarehe 25 hadi 31 Agost mwaka huu wa 2024 na kushiriki maadhimisho ya wiki ya tiba asilia kwa mwafrika yatakayofanyika Mkoani Mwanza.

Mganga Mkuu wa manispaa ya Bukoba Dkt Peter Mkenda. Picha na Theophilida Felician

Naye mganga Mkuu wa Manispaa ya Bukoba Dkt Peter Mkenda amewahimiza waganga wa Kagera wawatolee taarifa waganga wasio wa kweli ili kuziepuka shutuma mbalimbali zikiwemo mauaji.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Bukoba Dkt Peter Mkenda
Waganga na wakunga wa tiba asili mkoa wa Kagera wakiwa katika picha ya pamoja na katibu mkuu wa UWAWATA. Picha na Theophilida Felician

Nao baadhi ya waganga akiwemo bw.Fabiani Josephu na Abdu Majidi, Sospita na Sunati Ayubu kutoka Bukoba DC, Karagwe, na Manispaa ya Bukoba wamepongeza ujio wakatibu huyo wakidai kwamba ni mkombozi atakayethubutu serikalini ili kupata mwafaka mzuri wakuzitatua changamoto zao hivyo wameomba suala la Elimu kuenezwa zaidi kwa wananchi.

Baadhi ya waganga walioshiriki mkutano

Mfalme wa pili Dkt Prince Katega licha ya kuyabainisha mengi amesisitiza waganga kuungana pamoja na kutoa matamko yakukemea mambo ambayo yanaonekana kudidimiza uhai wa tiba asilia.

Katibu wa umoja huo mkoa wa Kagera Hatiani R. Kashobi ameshukuru na kupongeza ujio wakatibu mkuu Kagera ambao umekuwa chachu ya kuwaunganisha waganga wakawa kitu kimoja na imara.