Karagwe FM

Waganga wa tiba asili wadaiwa kuchochea mauaji, ubakaji Kagera

29 July 2024, 1:08 pm

Mkaguzi wa Jeshi la Polisi Bakari H.Mkonda akiongea na waganga wa tiba asili mkoa wa Kagera. Picha na Theophilida Felician

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera kupitia ofisi ya upelelezi limekutana na waganga wa tiba asili na viongozi wa kimila kujadili juu ya wimbi la vitendo vya uhalifu unaohusisha mauaji ya watu wenye ualbino na ubakaji wa watoto, yote yakihusishwa na imani za kishirikina

Na Theophilida Felician.

Imeelezwa kuwa kushamiri kwa watu wanaojiita waganga wa tiba asili na wapiga ramli chonganishi maeneo mbalimbali ya mkoa Kagera imekuwa moja ya sababu zinazotajwa kuchochea vitendo vya uhalifu wa mauaji yakiwemo ya watu wenye ualbino na ubakaji kwa watoto wadogo.

Akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Vyama vya Waganga wa Tiba Asili mkoa wa Kagera SHIVYATIATA lililofanyika katika manispaa ya Bukoba, mkaguzi wa jeshi la polisi ofisi ya upelelezi mkoa wa Kagera Bakari H. Mkonda amesema kuwa Kagera ni miongoni mwa mikoa yenye takwimu za juu katika makosa ya mauaji yakifuatiwa na ubakaji kwa watoto.

Ameeleza kuwa matukio ambayo yamekwisha jitokeza watuhumiwa wamekuwa wakihusisha matukio hayo na imani potovu za waganga hususani wapiga ramli chonganishi hivyo wanatakiwa kuripotiwa ili kuwabaini na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

Sauti ya mkaguzi wa jeshi la polisi Bakari H.Mkonda
Mwenyekiti wa taasisi ya Amani Kwanza mkoa wa Kagera bw. Maulid Rashid. Picha na Theophilida Felician

Abdu Ndenzako katibu wa waganga wilaya ya Karagwe na Kyerwa ameweka wazi ongezeko la waganga matapeli ambao wamekuwa na majina mengi yakiwemo maji moto, Sumbawanga, Kigoma na mengine mengi mara nyingi hawana makazi maalum na matokeo yake kwenda nyumba za kulala wageni na kutoa tiba maeneo hayo utaratibu ambao siyo mzuri.

Akiungwa mkono na mwenyekiti wa taasisi ya Amani Kwanza mkoa wa Kagera Bw. Maulidi Rashid, Ndenzako ameiomba serikalikutofumbia macho watu hao ambao wamekithiri kwani maeneo mbalimbali kwenye miti yamepambwa na vitambaa vyenye kuwatangaza.

Sauti ya Abdul Ndenzako na Maulid Rashid wakifafanua hatua za kuchukua kwa waganga matapeli
Mwenyekiti wa machifu na viongozi wa kimila mkoa wa Kagera bw. Hermes Peter Nyarubamba

Mwenyekiti wa Machifu na viongozi wa kimila mkoa Kagera Hermes Peter Nyarubamba amekemea vikali changamoto hiyo ya waganga hewa ambapo amehimiza watu wote kwa kushirikiana na serikali kuwachonjo katika kuwatolea taarifa kabla ya kuleta madhara zaidi kwa wananchi.

Vile vile baadhi ya waganga akiwemo Yustas Nyakubaho na Sadiki wamesema wazi kuwa wao kama waganga kutoa taarifa ni jambo linalowezekana japo kwa sasa imewawea vigumu maana taarifa ambazo wamewahi kuziripoti kwa baadhi ya askari wa jeshi la polisi zimekuwa zikivuja nakuwafikia wahusika hatimaye kuwapa vitisho vya kuwadhuru.

Baadhi ya waganga wakisisitiza hofu yao kwa polisi kuwapa taarifa za waganga matapeli

Baada ya maelezo hayo ya waganga mkaguzi wa polisi Bakari amewapa pole kwa kadhia hiyo huku akiwaelekeza kuwa iwapo wanataarifa wanaweza kuripoti kwa viongozi kadhaa akiwemo mkuu wa polisi wilaya, mkoa hata taifa pamoja na wakuu wa wilaya na mkoa.

Baadhi ya waganga wa tiba asili na viongozi wa kimila walioshiriki kikao na jeshi la polisi mkoa wa Kagera. Picha na Theophilida Felician

Jeshi la polisi mkoa wa Kagera limetoa wito wa kuwataka waganga halali wa tiba asilia kuwafichua waganga matapeli pamoja na wapiga ramli chonganishi ambao wameonekana kushamiri na kuhusishwa na matukio ya uvunjifu wa amani hususani mauaji ya watu wenye ualbino na ubakaji kwa watoto wadogo.