Karagwe FM

Mwenyekiti ALAT Taifa ahimiza usimamizi wa miradi ya maendeleo

26 July 2024, 9:19 pm

Mwenyekiti wa ALAT Taifa Murshid Ngeze akiongoza kikao mkoani Njombe. Picha na mwandishi wetu

Kamati tendaji ya Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania ALAT wamekutana wiki hii kujadiliana juu ya mambo mbalimbali ikiwemo kutoa maelekezo kwa mamlaka za serikali za mitaa juu ya usimamizi wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao

Na mwandishi wetu

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania ALAT Taifa Murshid Ngeze amewataka viongozi wa Jumuiya hiyo inayohusika moja kwa moja na miradi ya maendeleo ya wananchi, katika ngazi ya halmashauri kujikita katika kusimamia miradi ya maendeleo kwa kufanya ziara ya mara kwa mara ya kutembelea na kukagua utekelezwaji wa miradi hiyo ili ziwe ya tija kwa wananchi kama ilivyo kusudi la Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ngeze ameyasema hayo wakati wa kikao kazi cha kamati tendaji ya ALAT Taifa na viongozi wa mikoa, wenyeviti na makatibu iliyofanyika July 24.2024 Njombe Mji mkoani Njombe.

Amesema malengo mojawapo ya chombo hicho ni kusimamia miradi ya wananchi ili itekelezwe kwa weledi, ubora na kwa kuangalia thamani ya fedha na mwisho wananchi wapate huduma stahiki.

Aidha Ngeze amesema katika muktadha wa uhai wa Jumuiya hiyo wapo mbioni kuanzisha vitega uchumi vya ALAT vitakavyoisaidia kujiendesha bila kutegemea wahisani ili kuwa imara na kwenda kusimamia malengo yake kikamilifu.

Hata hivyo kikao hicho cha kamati tendaji ya ALAT Taifa na uongozi wa Jumuiya hiyo kimkoa ilihitimika kwa viongozi hao kufanya ziara katika mradi wa soko kuu la Njombe mji linalojengwa kwa zaidi shilingi bilioni 10 ambayo imetoa fursa kwa wafanyabiashara wasiopungua 680, na kutokana na utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa soko kuu la Njombe mji uongozi wa ALAT Taifa ukatoa pongezi kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyojikita katika kutekeleza miradi maendeleo katika mji wa Njombe .