Wachungaji wapiga ramli, washirikina waonywa Kagera
13 July 2024, 8:36 am
Baadhi ya viongozi wa dini nchini ni miongoni mwa kundi la wahalifu wanaokamatwa katika maeneo mbalimbali kutokana na chunguzi zinazofanywa na jeshi la polisi.
Miongoni mwa viongozi hao ni baadhi ya walimu wa madrasa wanaokamatwa wakituhumiwa kwa makosa ya ulawiti na ubakaji wa watoto akiwemo Bw. Abdallah Selemani (37), aliyehukumiwa kwenda jela miaka 30 mwezi Machi 2024 kwa kosa la kulawiti mwanafunzi wake wa kiume (12), pamoja na tukio la hivi karibuni la mauaji ya mtoto mwenye ualbino huko Kamachumu Muleba mkoani Kagera lililomhusisha Paroko msaidizi wa jimbo katholiki la Bukoba Elpidius Rwegoshora.
Na Respicius John
Viongozi wa dini mkoani Kagera wametakiwa kuacha tamaa ya fedha na matendo mengine ya aibu ili kuwaongoza waumini wao katika njia inayompendeza Mwenyezi Mungu.
Wito huo umetolewa na askofu wa jimbo la Kagera wa kanisa la Calvary Assemblies of God (CAG) Damian Dominic Rwabutikula wakati wa ibada ya kumsimika rasmi Bw. Dickson Rugaimukamu kuwa mchungaji wa kanisa hilo katika eneo la Kashaba Jogoma Kyaka wilayani Missenyi na kusema kuwa kanisa hilo liachukua hatua kwa kila mchungaji atakayebainika kukiuka maadili ya kazi yao
Afisa mtendaji wa kata ya Kyaka wilayani Missenyi bw. Egidius Ngirwa pamoja na kumpongeza bw. Dickson kwa kupata daraja la uchungaji amemuomba kufanya maombi kwa ajili ya eneo la Kyaka Jogoma alilodai limekithiri kwa uchafu wa kila aina ikiwemo wizi na migogoro ya kifamilia huku Bi Testuta Tibalila aliyemwakilisha mkuu wa wilaya ya Missenyi akitoa wito kwa waumini kudumisha amani na utulivu.
Mchungaji Dickson akapata fursa ya kuongea na hadhara iliyoshuhudia kusimikwa kwake kuwa mchungaji wa kanisa la CAG na akamshukuru Mungu kwa hatua hiyo na kuahidi kuendeleza karama yake ya kuimba sifa za Mungu kama alivyokuwa awali