BAWACHA Kagera yahimiza wanachama kujiandikisha kupiga kura
20 June 2024, 9:56 pm
Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA na jumuiya zake kimeendelea kutoa elimu kwa wananchi kujiandikisha na hatimaye kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Na Jovinus Ezekiel
Uongozi wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo BAWACHA mkoani Kagera wamehimiza wananchi na wanachama wa chama hicho wilayani Kyerwa kujitokeza na kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura kwa lengo la kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
Wakizungumuza katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika kata ya Isingiro wilayani Kyerwa mkoani Kagera kwa kuwakutanisha wanawake wa baraza la wanawake wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA mkoani Kagera viongozi wa baraza hilo wamesema kuwa wanawake wa chama hicho inabidi wawe mstari wa mbele katika kuhimiza wanachama na wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika kushiriki zoezi la kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura.
Miongoni mwa viongozi hao Devotha Nestory katibu wa baraza la wanawake BAWACHA mkoa wa Kagera na mwenyeki wa BAWACHA mkoani Kagera Magreth Kyai wamesema kuwa suala la wananchi kujiandikisha na kujitokeza kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ni muhimu katika kumchagua kiongozi atakayeteta shida za wananchi zinazowakabili katika maeneo yao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Kagera mwalimu Gration Mukoba kupitia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Isingiro amesema kuwa dira ya chama hicho ni kuhakikisha wananchi wananufaika na raslimali zinazotokana na nchi yao kwani mpaka sasa baadhi ya wananchi wanalalamikia ugumu wa maisha unatokana na kupanda kwa gharama za maisha ikiwa ni pamoja na uwepo wa changamoto za huduma za kijamii katika sekta ya maji, afya na miundo mbinu.
Hata hivyo ziara ya viongozi wa BAWACHA kwa mkoa Kagera imehitimishwa katika wilaya ya Ngara kwa kukutana na baadhi ya wanawake wa chama hicho ambao nao wametakiwa kuhakikisha wanashiriki zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ikiwa ni pamoja na kugombea nafasi mbalibali za uongozi husani ngazi ya vijiji na kata.