Karagwe FM

Madaktari bingwa wa Rais Samia waleta matumaini Kagera

19 June 2024, 9:39 pm

Afisa wa idara ya huduma za mama na mtoto kutoka wizara ya afya Bi. Grace Maliki. Picha na Theophilida Felician

Serikali kupitia wizara ya afya imeendelea na kampeni yake ya kusambaza huduma ya matibabu ya kibingwa kupitia huduma za mkoba kwa kutumia kambi maalum za madaktari bingwa katika halmashauri mbalimbali nchini. Awamu hii madaktari Bingwa wamepangwa na kuweka kambi ya matibabu mkoani Kagera

Na Theophilda Felician

Madaktari bingwa wa Rais Samia Suluhu Hassan waliofika Mkoani Kagera kwa ajili ya kutoa huduma ya matibabu ya kibingwa kwa wananchi wametajwa kuwa msaada mkubwa hasa kwa kuokoa gharama za kuwafuata katika hospitali kubwa zilizopo mbali na mkoa wa Kagera.

Ametoa kauli hiyo Afisa idara ya huduma za mama na mtoto kutoka wizara ya afya Bi. Grace Maliki kwenye uzinduzi wa huduma hiyo katika Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba akisema kuwa jumla ya madaktari 40 wamefika mkoani Kagera na kwamba kila Halmashauri imepangiwa madaktari watano watakaohudumu hadi Juni 21, 2024.

Amefafanua kuwa kampeni hiyo ya Rais Samia imelenga kuwasogezea huduma karibu na maeneo yao kwani waliowengi wamekuwa wakikosa huduma kutokana na uwezo mdogo wakutokuwa na gharama za kumudu safari ya kuzifuata zinakotolewa kutokana na umbali uliopo.

Afisa Maliki amesema kuwa tayari mikoa 23 kati ya mikoa 26 imehudumiwa na halmashauri 139 kati ya halmashauri 284 zimefikiwa.

“Serikali imeona vyema kuleta huduma hizo ili wananchi waweze kuzipata kwa ukaribu kabisa na kwa gharama nafuu” Ameeleza afisa Grace Maliki.

Aidha amewasihi wananchi wote mkoa wa Kagera wenye uhitaji wa matibabu kujitokeza katika hospitali zote za wilaya ili kuhudumiwa

Mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima.Picha na Theophilida Felician

Akiwakaribisha madaktari hao watakaokuwa Kagera kwa muda wa siku tano mkuu wa wilaya Bukoba Erasto Sima kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwasa amezitaja huduma zitakatolewa na madaktari hao ni pamoja na huduma kwa magonjwa ya wanawake na ukunga, upasuaji ubobezi wa mfumo wa mkojo, usingizi na ganzi, magonjwa ya ndani sambamba na magonjwa ya watoto.

Sima ameishukuru serikali kwa jitihada hizo muhimu, hivyo ametoa wito kwa watumishi wa afya kuwapa ushirikiano wa kutosha ili zoezi hilo liweze kukamilika vyema huku akiwasihi wananchi kutokukosa huduma kwani tayari imewafuata karibu.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Jocobo Simon naye ameishuru serikali na kuahidi kuwapa ushirikiano wa hali ya juu madaktari bingwa hao.

Baadhi ya madaktari wanaoshiriki kambi ya matibabu ya kibingwa katika manispaa ya Bukoba. Picha na Theophilida Felician

Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata tiba akiwemo Richard Rugaika mkazi wa mtaa wa Bushaga naye Happyenes Justasi kutoka mtaa wa Nshambya wameshukuru na kuwakaribisha madaktari kwani ni muda murefu wa kihangaika na matatizo yao ya magonjwa hivyo wamekuwa na matumaini ya kutatuliwa baada ya huduma hiyo kuwasogelea karibu.

Picha ya pamoja ya madaktari na viongozi wa serikali walioshiriki uzinduzi wa huduma za kibingwa manispaa ya Bukoba. Picha na Theophilida Felician