Karagwe FM

CHADEMA Kagera walia na sheria mbovu kwa wafanyakazi

8 June 2024, 6:14 pm

Mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA mkoa wa Kagera Gratian Mukoba. Picha na Mbuke Shilagi

Miongoni mwa mambo yanayolalamikiwa na watumishi wa umma nchini ni suala la kikokotoo cha mafao ya wastaafu ambacho wengi wa watumishi wanalalamikia sheria iliyopitishwa bungeni kuruhusu matumizi yake wakidai kuwa kina mapunjo ya mafao kwa wahusika.

Na Theophilida Felician Muleba.

Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Mkoa wa Kagera na rais mstaafu wa chama cha walimu nchini CWT Gration Mukoba amesema sheria zinazopitishwa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndizo zinazosababisha mambo mengi kutofanyika kwa weledi na kwa ufanisi.

Mukoba ameyabainisha hayo wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kitongoji cha Buhanga kata ya Buganguzi jimbo la Muleba kaskazini akifafanua kwamba kuna baadhi ya sheria zinazotungwa na wabunge kuwa kandamizi kwa wafanyakazi katika masuala kadhaa ikiwemo mishahara na kiinua mgongo.

“Wabunge wanavyokuwa wanapitisha sheria za ajabu ajabu na sheria mbovu wenyewe mbona hawajitungii? Wabunge wanapata kiinua mgongo baada ya miaka mitano na kiinua mgongo chao hakikatwi hata senti moja, walimu na wafanyakazi wengine wanapata kiinua mgongo chao baada ya miaka 30,33 hadi 40” Mukoba amefafanua.

Mbali na hayo amegusia changamoto kadhaa zinazoikabili sekta ya elimu hususani uhaba wa walimu kwa baadhi ya shule hali inayowalazimu walimu kufundisha kwa mzigo mkubwa wa wanafunzi madarasani ukilinganisha na uwiano wao.

Ametolea mfano wa shule ya msingi Biirabo alikosomea akisema kuwa enzi wao kila darasa lilikuwa na wanafunzi 45 madarasa 3 na walikuwa na walimu 13 jambo ambalo ni tofauti na sasa.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kukichagua chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA katika chaguzi zijazo ii kuyafanyia marekebisho yote yanayokumbatiwa na chama cha mapinduzi CCM na hatimaye kusababisha changamoto kwa umma.

Katibu cha chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA mkoa wa Kagera bw. Daniel Damian. Picha na Mbuke Shilagi

Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Kagera bw. Danieli Damian ni ameyataja mengi zaidi akikemea vitendo vya vitisho vilivyokwisha anza kujitokeza kwa wanachama hicho kutoka kwa wanachama wa CCM.

Amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanajiandikisha kwa wingi ili kuweza kuwachagua viongozi bora wa CHADEMA.

Mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Bukoba mjini bw. Chief Karumuna. Picha na Mbuke Shilagi

Hata hivyo Mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Bukoba mjini Chief Karumuna akiambatana na viongozi wenzake amezungumzia suala la serikali kutokuchukuwa hatua kwa watu wanaohusika kufanya ubadhirifu wa fedha za umma licha ya ripoti ya (CAG) kubaini huku akikemea tukio la kupotea kwa watu wawili tangu miaka miwili iliyopita katika kata Kishanda wilayani Muleba.

“Inasikitisha sana kuona tuna Serikali ambayo imeshindwa kulinda raia wake, tuna mtu anaitwa Mzee msukuma pale Kishanda ana watoto Amoni na Singi mnawafahamu tuna miaka miwili hawa watu hatunao, “Chiefu Karumuna

Baadhi ya wananchi wa kata ya Buganguzi wilayani Muleba wakiwa katika mkutano wa hadhara. Picha na Mbuke Shilagi