Halmashauri nne zaridhia mradi wa kuzuia ulemavu Kagera
1 June 2024, 10:48 am
Huduma za utengamao zinazotolewa kwa wenye ulemavu limekuwa hitaji kubwa kwa kundi hili ikizingatiwa kuwa mashirika yenye uwezo wa kutoa huduma hizi ni machache na yamekuwa na bajeti finyu. Kwa hali hiyo shirika lisilokuwa la kiserikali la Community Based Inclusive Development Organisation (CBIDO) limechukua dhamana ya kupanua huduma zake kutoka kuhudumia baadhi ya kata za wilaya ya Karagwe na kuongeza wilaya tatu za Kyerwa, Ngara na Missenyi
Na Jovinus Ezekiel.
Shirila lisilokuwa la kiserikali la CBIDO lililopo wilayani Karagwe mkoani Kagera limewakutanisha viongozi wa kisiasa kutoka wilaya za Ngara, Kyerwa, Karagwe na Missenyi hasa walioko katika ngazi za watoa maamuzi wilayani kwa ajili ya kujadili na kukubaliana kupanua huduma za utengamao kwa wenye ulemavu sambamba na kuzuia ulemavu siku za usoni.
Askofu wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kagera Darlingtone Bendankeha aliyeongoza kikao hicho katika ukumbi wa shirika la Beyond Inclusion (BI) eneo la Nyakanongo kata ya Kayanga wilayani Karagwe amesema kuwa mpango huu unatarajiwa kuanza mwezi Julai 2024 kwa wilaya hizo baada ya kuafikiana maeneo ya kuhudumia na kuweka mikakati ya kuzuia ulemavu ambapo pia mkurugenzi mtendaji wa CBIDO bw. Flourian Rwangoga alieleza walengwa wa huduma husika.
Wawakilishi wa madiwani katika halmashauri zote nne yaani Karagwe, Ngara, Kyerwa na Missenyi wamekubali kupokea mradi huo na kueleza kuwa utakuwa na manufaa zaidi kwa wenye ulemavu katika halmashauri zao kama alivyoanza kueleza makamu mwenyekiti wa Karagwe Dauson Byamanyirwohi aliyekiri kuwa halmashauri yake imenufaika na miradi ya CBIDO akifuatiwa na mwenyekiti wa halmashauri ya Missenyi Projestus Tegamaisho akiwakaribisha katika halmashauri ya Missenyi na kuwaahidi ushirikiano
Kupitia kikao hicho shirika la CBIDO limewaeleza wadau kuwa litatoa huduma kupitia mpango wa pamoja na kuwashukuru wenyeviti wa halmashauri husika kukubali na kupokea mradi huu