Lishe duni chanzo cha ongezeko la watoto njiti Karagwe
10 May 2024, 10:50 am
Mganga mkuu wa wilaya ya Karagwe Dkt Agnes Mwaifuge (katikati) akisisitiza jambo. Picha na Ospicia Didace.
Pamoja na mkoa wa Kagera kuwa na wingi wa vyakula, ni mmoja kati ya mikoa inayotajwa kuwa na utapiamlo pamoja na udumavu kutoka na wananchi kutozingatia matumizi sahihi ya vyakula hivyo.
Na Ospicia Didace
Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe mkoani Kagera Dkt.Agness Mwaifuge amewataka akina mama wajawazito kula vyakula vyenye lishe pamoja na kuhudhuria kliniki kwa wakati jambo litakalosaidia kukabiliana na changamoto ya akina mama hao kujifungua watoto njiti
Hayo yalisemwa na mganga mkuu wa wilaya ya Karagwe Dkt. Agness Mwaifuge ambaye ni katibu wa kikao cha kamati ya lishe kilichofanyika katika ukumbi wa Angaza mjini Kayanga wilayani Karagwe hivi karibuni akisema kuwa wilaya ya Karagwe kuna ongezeko la kuzaliwa watoto njiti huku akitaja changamoto kubwa kuwa ni ukosefu wa lishe kwa akina mama waja wazito.
Picha na Ospicia Didace
Dkt Mwaifuge amewataka wadau wa lishe kushirikiana kwa pamoja katika kutoa elimu kwa jamii juu ya mama mjamzito kupata mlo kamili pamoja na kupunguziwa kazi za nyumbani.
Naye mratibu wa lishe wilaya ya Karagwe bi Lustica Mgumba amezitaja changamoto zinazosababisha kuzaliwa kwa watoto njiti, midomo sungurua, mgongo wazi pamoja na magonjwa mengine kuwa ni pamoja na akina mama waja wazito kutotumia vidonge vya folic acid wakiamini kuwa vinaongeza damu wakati wa kujifungua jambo ambalo sio sahihi.
Akitoa maoni katika kikao hicho sheikh wa BAKWATA wilaya ya Karagwe Alhaj Nassib Abdul Abdallah amempongeza mratibu wa lishe kwa kusimamia vizuri idara hiyo kwa kutoa elimu katika ngazi ya kijiji ambapo pia amewahimiza wadau wa lishe kuendelea kutimiza wajibu wao ili kusaidia jamii kuzingatia lishe kwa usahihi