Chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kuwafikia watoto wa kike Karagwe
20 April 2024, 4:30 pm
Wizara ya afya nchini imekuwa na desturi ya kuzuia magonjwa hasa yale yanayozuilika kwa chanjo kupitia kampeni maalum za chanjo kwa watoto wadogo ambapo mara hii inaendesha kampeni ya siku tano kuwachanja wasichana wenye umri wa miaka 9-14 kuwakinga dhidi ya saratani ya shingo ya mlango wa kizazi.
Na Ospicia Didace.
Halmashauri ya wilaya ya Karagwe kupitia Idara ya Afya inatarajia kutoa chanjo kwa watoto wa kike zaidi ya 33,720 wenye umri wa miaka 9-14 kupitia kampeni ya siku tano kuanzia Aprili 22, 2024.
Kwa mujibu wa mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe Dk. Agnes Mwaifuge akiwa katika kikao cha kamati ya afya ya msingi PHC hivi karibuni katika ukumbi mdogo wa ofisi ya mganga mkuu wilaya ya wilaya ya Karagwe Nyakanongo kampeni hii itafanyika wilayani kote Aprili 22 hadi 26, 2024 na kwamba itaendelea hadi Desemba mwaka huu kwa lengo la kuhakikisha watoto lengwa wanapokea chanjo hizo
Naye mwenyekiti wa kikao Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Julius Laiser ameitaka Idara ya Afya kuendelea kutoa elimu juu ya usahihi wa chanjo na kukemea baadhi ya wananchi wanaoendekeza imani potofu.
Mkuu wa Wilaya amewasisitiza wajumbe kupeleka ujumbe wa kuhamasisha jamii kuleta watoto wenye sifa wapate chanjo kwani mtaji na mafanikio ya kila binadamu ni afya yake.
Amesema kuwa timu za wachanjaji zitapita katika maeneo yenye mikusanyiko kama vile misikitini, makanisani, sokoni na kwingineko ili kukidhi matakwa ya mkoa wa Kagera kuchanja wasichana wenye umri wa miaka 9-14 wapatao 271,650