Mabweni matatu Missenyi yapokea shilingi Milioni 517.8
16 February 2024, 5:45 pm
Halmashauri ya wilaya ya Missenyi imeweka utaratibu wa kufuatilia hali ya utekelezaji wa miradi iliyopokea fedha za serikali kila robo ambapo kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/2024 wameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya elimu afya na maji
By Shabani Ngarama
Jumla ya shilingi milioni 517.84 zimetumika katika ujenzi wa mabweni ya shule tatu za sekondari wilayani Missenyi kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/2024
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kamati za ujenzi kwa kamati ya fedha uchumi na mipango ya halmashauri ya wilaya hiyo hivi karibuni, shilingi milioni 479,844,500 zilitolewa na serikali na shilingi milioni 92 ni michango ya wadau wa maendeleo wa kata ya Bwanjai waliochangia ujenzi wa bweni la shule ya sekondari Bwanjai lenye uwezo wa kulaza wanafunzi wa kike 80 na lipo katika hatua ya ukamilishaji na kuwekewa samani. Hadi sasa bweni hilo limetumia shilingi milioni 142,844,500 kabla ya kukamilika na kutumika
Pamoja na bweni hilo kufadhiliwa na wananchi wa kata ya Bwanjai waishio ndani na nje ya kata hiyo wanafunzi wa shule hiyo pia walinufaika na msaada wa vitabu vya tahakiki kwa ajili ya kujiandaa na mitihani ya kitaifa ya kidato cha pili na nne na vitabu hivyo vilikabidhiwa kwao na diwani wa kata ya Bwanjai Phocas Rwegasira mbele ya wajumbe wa kamati ya fedha uchumi na mipango
Ukiachilia mbali bweni la shule ya sekondari Bwanjai, halmashauri ya wilaya ya Missenyi imetoa shilingi milioni 130 kujenga bweni katika shule ya sekondari ya Minziro kata ya Minziro yenye kidato cha kwanza hadi cha sita, shilingi milioni 205 kwa ajili ya ujenzi wa bweni katika shule ya sekondari Kagera kata ya Kyaka ambayo pia mwezi Julai mwaka huu imepanga kupokea wanafunzi wa kidato cha tano. Pia shilingi milioni 40 zilitolewa kwa shule ya sekondari ya kidato cha kwanza hadi cha sita ya Bunazi kata ya Kassambya kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa bweni la wasichana shuleni hapo na uzio huo uko katika hatua za ukamilishaji
Akiongea na chombo hiki baada ya kukamilisha ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi bw. Projestus Tegamaisho alisema kuwa miradi ya elimu pia imeenda sambamba na miradi ya afya na maji na kuongeza kuwa walikagua na kuridhika na utekelezaji wa miradi na matumizi ya fedha ya serikali. Ameitaja miradi mingine kuwa ni mradi wa maji wa Kanyigo iliyogharimu shilingi bilIONI 1.8 fedha za EP4R, Mradi wa ukamilishaji wa kituo cha afya Kanyigo kwa shilingi milioni 30 za mapato ya ndani, ununuzi wa tenki na ujenzi wa mnara wa tenki la maji Zahanati ya Kanyigo, ujenzi wa matundu matano ya choo cha Zahanati kwa shilingi milioni 94.2 zilizotolewa na serikali kuu kwa ufadhili wa mradi wa WASH pamoja na shamba la ekari 7 za kahawa kata ya Kashenye na ukarabati wa mwalo wa Kabindi kwa thamani ya shilingi milioni 5. Na miradi yote hii ipo kwenye hatua ya umaliziaji katika tarafa ya Kiziba.
Sauti ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Missenyi Projestus Tegamaisho akielezea mradi wa shamba la kahawa lenye ukubwa wa ekari saba
Kwa upande wa tarafa ya Missenyi miradi yenye thamani ya shilingi milioni 870.2 ilikaguliwa na kamati hiyo na kuridhishwa na thamani ya fedha iliyotumika ambapo pamoja na mambo mengine halmashauri iliahidi kuongeza fedha kwa ajili ya kukamilisha mapungufu ya kibajeti yaliyojitokeza. Pia kamati ilipokea changamoto za soko la Bunazi na kuahidi kutumia shilingi bilioni 1 zilizopangwa kwenye bajeti ya mwaka 2024/2025 kuondoa changamoto hizo.
Miradi yote iliyotembelewa na kamati ya fedha uchumi na mipango ina gharama ya shilingi bilioni 2 na milioni 870.2