Zenj FM
Zenj FM
10/04/2026, 14:35

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Fahad Soud Hamid, amesema mikopo na uwezeshaji imeongezeka kwa asilimia 28, huku faida kabla ya kodi ikipanda kwa asilimia 20 kutokana na kuimarika kwa mapato na udhibiti wa matumizi. Aidha, benki imepanua huduma zake na inaendelea kujipanga kuwekeza zaidi katika teknolojia na kuboresha huduma kwa mwaka 2026.
Na Mary Julius.
Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) imeandika historia mpya ya mafanikio baada ya kuongeza rasilimali zake kwa asilimia 10, kufikia shilingi trilioni 2.75 mwaka 2025 kutoka trilioni 2.5 mwaka 2024 hatua inayoashiria uimara mkubwa wa kifedha na kuimarika kwa nafasi yake kama mhimili wa maendeleo ya uchumi Zanzibar.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki hiyo Fahad Soud Hamid, ameyasema hayo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya mafanikio ya benki hiyo na taarifa rasmi ya hesabu za benki kwa mwaka 2025 katika ukumbi wa Benki hiyo Mperani, amesema mafanikio hayo yanaipa benki nguvu zaidi ya kupanua huduma za mikopo na uwezeshaji kwa wananchi na sekta mbalimbali za kiuchumi.
Amesema mikopo na uwezeshaji kwa ujumla umefikia trilioni 1.55 mwaka 2025 kutoka trilioni 1.21 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 28.
Kati ya hizo, trilioni 1.15 ni mikopo ya kawaida huku bilioni 409 zikiwa ni uwezeshaji unaofuata misingi ya sharia kupitia PBZ Ikhlas.
Kwa upande wa ubora wa mikopo, amesema uwiano wa mikopo chechefu umeshuka hadi asilimia 1.95, kiwango kilicho chini ya ukomo wa asilimia 5 uliowekwa na msimamizi wa mabenki.
Katika uwekezaji, benki hiyo imeongeza uwekezaji kwenye hati fungani za serikali kwa asilimia 35, kufikia bilioni 222 mwaka 2025 kutoka bilioni 164 mwaka 2024.
Aidha, amana za wateja zimeongezeka kutoka trilioni 1.95 hadi trilioni 2.26, sawa na ongezeko la asilimia 16, ambapo trilioni 1.67 ni amana za kawaida na bilioni 578 ni za wateja wa huduma za Kiislamu.
Kwa upande wa faida kabla ya kodi, PBZ imepata bilioni 110.2 mwaka 2025 kutoka bilioni 92 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 20.
Ongezeko hilo limechangiwa na kuimarika kwa mapato ya mikopo, uwezeshaji pamoja na udhibiti mzuri wa gharama za uendeshaji.
Kutokana na mafanikio hayo, mtaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umeongezeka kwa asilimia 27 hadi kufikia bilioni 314 kutoka bilioni 248 mwaka uliopita.
PBZ pia imeendelea kuimarika katika vigezo vyote vya kifedha vinavyohitajika, ikiwemo mtaji na ukwasi, hali inayoonesha uimara endelevu wa benki hiyo.
Katika kuboresha huduma, benki hiyo imepanua mtandao wake na kufikia zaidi ya vituo 50 vya huduma, ikiwa ni pamoja na kufungua vituo vipya Kiwengwa, Konde na Madungu, pamoja na tawi jipya mkoani Arusha.
Akizungumzia mipango ya mwaka 2026, Mkurugenzi huyo amesema PBZ inalenga kuwekeza zaidi katika teknolojia za kisasa, kuimarisha usalama wa mifumo ya kifedha, kuzindua huduma ya Corporate Portal, pamoja na kuanzisha matawi yanayotembea Unguja na Pemba.
Aidha, ameahidi kuendelea kuboresha huduma kwa wateja kwa kuongeza uwazi na ufanisi katika utendaji kazi.
Mkurugenzi Fahad amezipongeza serikali zote mbili kwa mchango wao katika mafanikio hayo, akibainisha kuwa sera nzuri zimechangia ukuaji wa benki hiyo.
Amewapongeza wateja wa PBZ kwa kuendelea kuiamini na kuitumia, huku akiahidi kuwa benki hiyo itaendelea kuboresha huduma zake ili kudumisha ubora na ushindani wake.