Zenj FM
Zenj FM
07/04/2026, 23:20

Mbunge wa Fuoni, Asha Hussein Saleh, ameahidi kushirikiana na Wizara ya Vijana na Michezo kuendeleza michezo ya bao na drafti nchini. Amesema vipaji vingi vipo na tayari baadhi ya wachezaji wanafanya vizuri kimataifa.
Na Mary Julius.
Mbunge huyo amesema kuwa michezo hiyo tayari inachezwa katika nchi mbalimbali nje ya Tanzania, na baadhi ya washiriki wamefanikiwa kuleta makombe nchini, jambo linalodhihirisha kuwa kuna vipaji vingi vinavyohitaji kuendelezwa.
Mbunge Asha ameyasema hayo mara baada ya kukamilika kwa mashindano ya drafti na bao yaliyofanyika Fuoni Kiembeni yaliyojumuisha washiriki kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. Mashindano hayo yaliandaliwa kwa lengo la kumuenzi muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, Hayati Mzee Abeid Amani Karume, ambaye alipenda michezo hiyo
Asha amesisitiza kuwa mashindano hayo yataendelea kufanyika kila mwaka chini ya udhamini wake, kwa lengo la kuimarisha michezo hiyo na kutoa fursa zaidi kwa vijana kushiriki na kuonyesha vipaji vyao.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendeleza misingi ya upendo, umoja na undugu waliyoachiwa na viongozi waasisi wa taifa la Tanzania, Hayati Abeid Amani Karume na Hayati Julius Nyerere.
.Akizungumza baada ya ushindi wake, mshindi wa kwanza wa mchezo wa drafti, Saidi Hamisi kutoka Dar es Salaam, amesema mashindano hayo yalikuwa na ushindani mkubwa.

Kwa upande wake, mshindi wa pili Mohammed Saidi kutoka Zanzibar amesema mashindano yalikuwa ya kuvutia na yenye ushindani mkubwa, akibainisha kuwa mshindi wa kwanza alikuwa amejiandaa vyema zaidi.
Aidha amewahamasisha vijana kuendelea kufanya mazoezi ili kuboresha viwango vyao.
Naye Hamza Kasim amesema kuwa mchezo wa drafti haujapewa kipaumbele kinachostahili, akitoa wito kwa serikali na wadau mbalimbali kuudhamini ili kufungua zaidi fursa kwa vijana na kuukuza mchezo huo.
Katika mashindano hayo washindi walipata fedha taslim , vikombe pamoja na medali.