Zenj FM

Changamoto ya umeme Zanzibar kubaki historia

25/03/2026, 16:32

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dk Juma Malik Akil akizungumza mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea miradi ya kimkakati  ya maendeleo kwa sekta ya umeme wa jua na upepo katika Mkoa wa Kusini Unguja.

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Juma Malik Akil, amesema Zanzibar itapata umeme wa uhakika ndani ya miezi michache ijayo kutokana na miradi mipya ya nishati. Amesema serikali inawekeza katika umeme wa jua na upepo ili kuongeza uzalishaji hadi megawati 500 na kupunguza utegemezi wa chanzo kimoja.

Na Mary Julius.

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Juma Malik Akil amesema kuwa ndani ya miezi michache ijayo Zanzibar itakuwa na umeme wa uhakika, kufuatia juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Nane katika kuimarisha sekta ya nishati ya umeme nchini.

Akizungumza mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea miradi ya kimkakati  ya maendeleo kwa sekta ya umeme wa jua na upepo katika Mkoa wa Kusini Unguja, Waziri juma amesema kwa sasa Zanzibar inategemea chanzo kimoja cha umeme, hali ambayo ni hatari kwa maendeleo endelevu ya uchumi.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo mipya unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa hadi megawati 500, hatua itakayochochea uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo viwanda na hoteli.

Amesisitiza kuwa serikali imejipanga kikamilifu kwa  kugharamia miradi hiyo ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi kwa manufaa ya wananchi.

Aidha, Waziri huyo amesema kabla ya kuanza kwa bajeti mpya, serikali inaendelea kufanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita ili kupima mafanikio yaliyopatikana na kubaini maeneo ya kuboresha zaidi.

Sauti ya Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Juma Malik Akil.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Nishati na Madini Nadir Abdul latif Alwardi  amesema serikali imetenga fedha za kutosha kuhakikisha changamoto ya umeme Zanzibar inakuwa historia ifikapo mwaka 2028.

Sauti ya Waziri wa Maji, Nishati na Madini Nadir Abdul latif Alwardi.

Naye Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar, Mhandisi Haji Haji, amesema lengo la ziara hiyo ni kukagua maendeleo yaliyofikiwa katika sekta ya umeme. Ameongeza kuwa tangu Rais wa Zanzibar aingie madarakani, juhudi kubwa zimefanyika katika sekta mbalimbali ikiwemo nishati.

Hata hivyo, amebainisha kuwa ongezeko la matumizi ya umeme ni changamoto kubwa, ambapo kwa sasa Zanzibar inapokea megawati 135.7 huku mahitaji yakiwa megawati 165, hali inayosababisha upungufu wa umeme.

Amesema kukamilika kwa miradi hiyo mipya kutasaidia kuzalisha umeme wa kutosha, kupunguza uhaba uliopo na kuwezesha upatikanaji wa huduma ya umeme wa uhakika kwa wananchi wote.

Sauti ya Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar, Mhandisi Haji Haji.

Ziara hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika mwaka wa fedha 2025/2026.