Zenj FM
Zenj FM
15/03/2026, 19:48

Na Mary Julius.
Ahadi hiyo ameitoa katika futari iliyoandaliwa na Skuli ya Kiponda kwa wanafunzi walioko kambini wakijiandaa na mitihani yao. Amesema motisha hiyo inalenga kuwahamasisha wanafunzi kusoma kwa bidii ili waweze kusaidia familia na jamii yao.
Mbunge wa Jimbo la Malindi, Muhsin Haji Ussy, amewaahidi zawadi wanafunzi wa kidato cha sita watakaofaulu kwa daraja la kwanza na la pili katika mitihani yao ya taifa, ikiwa ni pamoja na kuwapatiwa kompyuta pamoja na kuwaalika kutembelea Bunge.
Mbunge huyo ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza katika futari iliyoandaliwa na Skuli ya Kiponda kwa ajili ya wanafuzi wa kidato cha sita ambao kwa sasa wako kambini wakijiandaa na mitihani ya taifa.
Amesema lengo la motisha hiyo ni kuwahamasisha wanafunzi kusoma kwa bidii ili waweze kuwa wakombozi wa familia zao na jamii kwa ujumla.
Kutokana na mafanikio ya maandalizi ya futari hiyo, Mbunge Musini amewashauri wanafunzi na walimu wa skuli hiyo kuanzisha kampuni ndogo ya upishi ili waweze kupata fursa ya kupokea oda za chakula na kujiongezea kipato.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Kiponda Miza Kai Khamisi amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwajalia kufanikisha futari hiyo kwa ajili ya wanafunzi waliopo kambini, hatua ambayo imewapa faraja na kuwafanya wajisikie vizuri wakati wa maandalizi ya mitihani.
Aidha amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Malindi, kamati ya skuli pamoja na wadau wote waliofanikisha futari hiyo, akisema imekuwa chachu na motisha kwa wanafunzi wanaojiandaa na mitihani ya taifa.
Naye mmoja wa wanafunzi walionufaika na futari hiyo amesema tukio hilo limewapa moyo na kuwahamasisha kufanya vizuri zaidi katika masomo yao ili kufikia malengo yao ya kielimu.