Zenj FM

Waziri wa Fedha Zanzibar azungumzia nafasi ya NCBA katika kukuza uchumi

12/03/2026, 19:41

Kaimu Mkurugenzi NCBA Rahim Suleiman akimkabidhi zawadi Waziri wa Fedha Zanzibar Dkt Juma Malik Akilm katika hafla ya futari iliyoandaliwa na benki hiyo.

Na Mary Julius.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Juma Malik Akil ameipongeza NCBA Bank kwa mchango wake mkubwa katika kukuza sekta ya fedha na kuchochea maendeleo ya uchumi wa visiwa vya Zanzibar.

Akizungumza katika hafla ya futari iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wadau wa biashara na wateja wake katika Hotel Verde Zanzibar, Waziri huyo amesema taasisi za kifedha zina nafasi muhimu katika kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Amesema kuwa kama mmoja wa wateja wa benki hiyo, ameshuhudia namna ilivyoweza kuvutia na kuongeza wateja kutoka sekta mbalimbali, hatua inayochangia kukuza shughuli za kiuchumi na kuongeza fursa za uwekezaji.

Waziri Malik amesisitiza kuwa maendeleo ya Zanzibar yanategemea zaidi ubunifu, matumizi sahihi ya akili na rasilimali zilizopo, kutokana na ukweli kwamba visiwa hivyo vina eneo dogo la ardhi.

Aidha ametoa wito kwa benki hiyo kuendelea kupanua wigo wa huduma zake na kuimarisha ushirikiano na Serikali pamoja na sekta binafsi ili kuchochea uwekezaji na kuharakisha maendeleo ya uchumi.

Sauti ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Juma Malik Akil.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi NCBA Rahim Suleiman amesema lengo la mkutano huo halikuwa tu kufutari pamoja, bali pia kuimarisha umoja, amani na mshikamano kati ya wateja, wafanyabiashara na wawekezaji.

Aidha Rahim amesema NCBA Bank inaamini katika ushirikiano wa kibiashara unaosaidia kukuza uchumi wa watu binafsi na jamii kwa ujumla.

Aidha imeahidi kuendelea kusimama pamoja na wateja wake, wafanyabiashara na wawekezaji kwa kuwapatia huduma za kifedha na mitaji hata katika kipindi hiki cha Ramadhani ambapo shughuli za biashara zinaendelea kama kawaida.

Sauti ya Kaimu Mkurugenzi NCBA Rahim Suleiman.

Kwa upande wake, Meneja Masoko wa NCBA Bank, Solomoni Frank, amesema benki hiyo imejipanga kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika juhudi za kukuza uchumi na kuimarisha maendeleo ya sekta ya fedha visiwani humo.

Sauti ya Meneja Masoko wa NCBA Bank, Solomoni Frank.