Zenj FM

Puma Energy yahakikisha upatikanaji wa mafuta haukatiki Zanzibar

07/03/2026, 17:44

Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Nadir Abdullatif Al‑wardy, akizungumza wakati wa futari iliyoandaliwa na kampuni ya Puma Energy iliyofanyika Golden Tulip Zanzibar Airport Hotel.

Na Mary Julius.

Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Nadir Abdullatif Al‑wardy,amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dk Hussein Ali Mwinyi imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha nishati ya mafuta inaendelea kupatikana kwa uhakika kwa wananchi pamoja na sekta mbalimbali za uchumi.

Waziri huyo ameyasema hayo wakati wa futari iliyoandaliwa na kampuni ya Puma Energy iliyofanyika katika Golden Tulip Zanzibar Airport Hotel, amewataka wananchi wa Zanzibar kuondoa wasiwasi kuhusu upatikanaji wa mafuta, akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha nishati hiyo muhimu haipungui licha ya changamoto za kimataifa zinazotokana na migogoro ya vita inayoendelea duniani.

Waziri Al-wardy pia ameishukuru kampuni ya Puma Energy kwa mchango wake katika sekta ya nishati nchini, akieleza kuwa ni kampuni inayotekeleza majukumu yake kwa ufanisi na ambayo Serikali ina imani nayo.

Ameitaka kampuni hiyo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha upatikanaji wa nishati, pamoja na kuandaa shughuli kama hiyo pia katika kisiwa cha Pemba.

Sauti ya Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Nadir Abdullatif Al‑wardy.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatuma Abdalla, ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yameiwezesha kampuni hiyo kuendelea kuwekeza na kupanua huduma zake.

Amesema kampuni hiyo ina mipango mbalimbali ikiwemo kuleta nishati safi ya kupikia ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanatumia nishati safi ya kupikia, ikiwa ni utekelezaji wa lengo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kufikia asilimia 80 ya wananchi kutumia nishati hiyo.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatuma Abdalla.

Aidha, amesema kampuni hiyo imejipanga kukabiliana na changamoto za hali ya kimataifa ili kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea bila kukatika kwa wateja wake.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatuma Abdalla.

Naye Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Mahmoud Mussa Wadi, amesema tukio hilo limekuwa fursa muhimu ya kuikumbusha jamii kuwa kuwafuturisha waliofunga ni miongoni mwa matendo yenye fadhila kubwa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Sauti ya Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Mahmoud Mussa Wadi