Zenj FM
Zenj FM
04/03/2026, 18:07

Na Mary Julius.
Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Zanzibar, Nadir Abdullatif Alwardy amesema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za maji, umeme na nishati kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi wa Unguja na Pemba.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo kuhusu siku 100 za mafanikio ya uongozi wa awamu ya pili ya Dkt. Mwinyi, kwa upande wa sekta ya maji, Waziri amesema Mradi wa Uimarishaji wa Miundombinu ya Maji Kengeja – Kisiwani Pemba umekamilika na kuunganisha zaidi ya nyumba elfu moja mia moja hamsini, hatua iliyomaliza changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi katika eneo hilo.
Aidha, kupitia mradi unaofadhiliwa na Benki ya EXIM ya India, kaya elfu kumi na saba mia saba ishirini na sita katika maeneo mbalimbali ya Unguja zimeunganishwa na huduma ya maji safi na salama majumbani.
Waziri amesema Serikali pia imefanikiwa kurejesha huduma ya maji katika maeneo yaliyoathiriwa na ujenzi wa barabara, kurekebisha mivujo themanini na tisa ya mabomba, kuweka zaidi ya kilomita kumi na tano za mabomba mapya pamoja na kusafisha visima kumi na vinne ili kuongeza uzalishaji wa maji.
Kwa upande wa nishati, Waziri amesema vijiji kumi na saba vimepatiwa umeme na wateja wapya elfu kumi na nane mia tano arobaini na nane wameunganishwa, sawa na asilimia mia moja na kumi ya lengo lililowekwa.
Amesema Serikali kupitia Shirika la Umeme Zanzibar imebadilisha nguzo mbovu, kukagua transfoma na kuboresha miundombinu ili kupunguza hitilafu za umeme.
Kutokana na ongezeko la mahitaji ya umeme, Waziri amesema Serikali imeidhinisha mradi wa waya mpya wa baharini utakaokuwa na uwezo wa megawati mia mbili sabini kwa Unguja na megawati mia moja kwa Pemba, mradi unaotarajiwa kuimarisha uhakika wa umeme kwa muda mrefu.
Katika sekta ya mafuta na gesi, Waziri amesema lita milioni mia moja sitini za mafuta zimeingizwa nchini pamoja na kilogramu milioni saba nukta tatu za gesi ya kupikia.
Ameeleza kuwa changamoto ya muda mfupi ya uhaba wa mafuta imetatuliwa na hali ya upatikanaji sasa ni shwari.
Serikali imeendelea kusisitiza udhibiti wa bei za mafuta na gesi ili kulinda wananchi dhidi ya mabadiliko ya bei katika soko la dunia.
Waziri ametoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu ya maji na umeme, kulipa bili kwa wakati na kushirikiana na Serikali katika kulinda rasilimali za Taifa.