Zenj FM
Zenj FM
19 February 2026, 4:33 pm

Na Mary Julius.
Afisa Saikolojia wa Wizara ya Afya, Dkt. Mussa Khamisi Juma, amewataka wanafunzi wanaoshiriki mashindano ya Qur’an kujiepusha na vitendo vyovyote vya kihalifu na kuzingatia maadili mema yanayowajenga katika misingi ya dini.
Dkt. Juma ameyasema hayo wakati akitoa nasaha katika mashindano ya 13 ya Qur’an yaliyoandaliwa na Skuli ya Kiponda.
Amesema elimu wanayoipata inapaswa kuwajenga katika mazingira ya kumcha Mwenyezi Mungu, kusoma kwa ajili ya Allah na kuutumikia Uislamu kwa vitendo vyema.
Aidha, amewapongeza walimu wa Skuli ya Kiponda kwa kuandaa mashindano hayo, akieleza kuwa yanasaidia kuwajenga na kuwalea vijana katika misingi imara ya imani na maadili ya dini.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Kiponda, Miza Kai Khamis, amesema mashindano hayo yameandaliwa kwa lengo la kuendeleza mafunzo ya kusoma na kuyafanyia kazi yale yote yaliyoandikwa katika Kitabu Kitukufu cha Qur’an, kama alivyoamrisha Allah (Subhanahu wa Ta’ala). Ameeleza kuwa mantiki ya mashindano hayo ni kuwajenga watoto kuwa wema na kuwa viongozi waadilifu wa taifa siku za usoni.
Mwalimu Mkuu huyo pia amemuomba Mbunge wa jimbo la Malindi kuwa mlezi wa skuli hiyo, akibainisha kuwa kuna mahitaji mengi ikiwemo kusaidia wanafunzi wasio na uwezo wa kulipia gharama za kambi.
Amesema kati ya wanafunzi 102 wa skuli hiyo, ni wanafunzi 80 pekee waliofanikiwa kuhudhuria kambi, huku matarajio yakiwa ni kuwawezesha wanafunzi wote kushiriki.
Kwa upande wao, wanafunzi walioshinda katika mashindano hayo wamewahimiza wenzao kuongeza juhudi katika kuisoma Qur’an na kuwasikiliza walimu wao ili waweze kuelewa vyema mafunzo wanayopatiwa.