Zenj FM

Baraza la Wawakilishi lawanoa waandishi

15 February 2026, 8:56 am

Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Hudhaima Mbarak Tahir.

Na Mary Julius.

Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Hudhaima Mbarak Tahir, amewataka waandishi wa habari kuzingatia maadili ya taaluma yao, kuthibitisha taarifa kabla ya kuzichapisha au kuzitangaza, ili kuepuka upotoshaji unaoweza kuleta taharuki au mgawanyiko katika jamii.

 Hudhaima ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo maalum kwa waandishi wa habari yaliyofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, ambapo amesisitiza kuwa vyombo vya habari vina jukumu kubwa katika kuhabarisha umma na kujenga jamii yenye uelewa sahihi wa masuala ya kitaifa.

Amesema ni muhimu kwa wanahabari kutumia taaluma na ujuzi wao ipasavyo katika kuwasilisha taarifa kwa usahihi, uwazi na uwajibikaji, akibainisha kuwa taarifa sahihi na zenye ukweli huchangia kuimarisha misingi ya demokrasia na kuchochea maendeleo endelevu ya taifa.

Aidha, amewahimiza waandishi kuendelea kushirikiana na taasisi za umma katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sera na mipango ya Serikali, kwa lengo la kuongeza uelewa, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika masuala ya maendeleo.

Sauti ya Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Hudhaima Mbarak Tahir.

Kwa upande wake  Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Issa Mselem, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uelewa waandishi wa habari juu ya kuripoti kwa usahihi habari za Baraza la Wawakilishi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kuhabarisha umma kwa ufanisi.

Sauti ya Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Issa Mselem.

Akizungumza kwa niaba ya waandishi wa habari mwandishi mkongwe Salim Salim ameushukuru uongozi wa Baraza kwa kuandaa mafunzo hayo, ambayo yamekuwa na msaada mkubwa kwa waandishi chipukizi na wakongwe katika kuboresha uandishi wao na kuzingatia maadili ya taaluma.

Aidha, ameomba mafunzo kama hayo yaandaliwe mara kwa mara ili kuendelea kuboresha uandishi wa habari za Baraza na kuhakikisha umma unapata taarifa sahihi, zenye uwiano na zenye tija.

Sauti ya Mwandishi mkongwe Salim Salim.

Katika mafunzo hayo, mada tatu ziliwasilishwa, zikiwemo: Muundo wa Baraza la Kumi na Moja la Wawakilishi la Zanzibar na misamiati maarufu inayotumika katika uendeshaji wa shughuli za Baraza; Taratibu za Utekelezaji wa Kazi na Majukumu ya Baraza la Wawakilishi; pamoja na Uibuaji na Uandishi wa Habari za Baraza.