Zenj FM
Zenj FM
13/02/2026, 20:44

Wazazi na walezi wametakiwa kuhakikisha wanawaandikisha shule mapema watoto wenye mahitaji maalum, mara tu wanapofikia umri wa kuanza masomo ili wapate haki yao ya msingi ya elimu sawa na watoto wengine.
Na Hakika Mwinyi.
Wito huo umetolewa na Afisa Elimu Wilaya ya Kati, Somoe Said Mussa, wakati wa kikao cha tathmini ya uandikishaji wa wanafunzi wapya wa ngazi ya Maandalizi na Msingi kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Elimu Kidimni.
Amesema kuwa kwa mwaka 2026, idadi ya wanafunzi walioandikishwa katika ngazi ya Maandalizi na Msingi imeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2025.
Ameeleza kuwa ongezeko hilo limetokana na jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na wadau wa elimu kuhakikisha watoto wote waliofikia umri wa kusoma wanaandikishwa kwa wakati.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Taaluma wa Skuli ya Tunguu, Sabra Said Sultan, amewataka wazazi kushirikiana kwa karibu na walimu, ikiwemo kufuatilia maendeleo ya watoto wao na kutambua changamoto wanazokabiliana nazo wakiwa shuleni.
Naye Mwenyekiti wa Skuli ya Chwaka, Vuaa Mwadini Mcha, amewaomba walimu kuweka utaratibu maalum wa mikutano ya pamoja kati ya wazazi, walimu na wanafunzi ili kujadili maendeleo ya kielimu na ustawi wa watoto.
Jumla ya washiriki 74 walihudhuria mkutano huo wa tathmini ya uandikishaji wa wanafunzi wa ngazi ya Maandalizi na Msingi katika skuli za Wilaya ya Kati, wakiwemo mwakilishi wa TC, mkaguzi wa elimu, walimu wa taaluma, wenyeviti wa skuli pamoja na masheha.