Zenj FM

Jamii yahimizwa kujiunga na bima ya Takaful kuepuka mifumo ya riba

12 February 2026, 4:39 pm

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZIC Takaful, Said Abdallah Sleyum akizungumza wakati wa mafunzo maalum kwa viongozi wa jumuiya za Kiislamu Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Na Mary Julius.

Jamii imetakiwa kujitokeza kwa wingi na kutumia huduma za bima ya Takaful ili kujiepusha na mifumo ya riba iliyokatazwa katika mafundisho ya dini.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZIC Takaful, Said Abdallah Sleyum, wakati wa mafunzo maalum kwa viongozi wa jumuiya za Kiislamu Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Walimu Kaskazini Unguja, yamelenga kutoa elimu juu ya mfumo wa bima ya Takaful na umuhimu wake kwa jamii, hususan kwa kuzingatia misingi ya Sharia.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Sleyum amesema vitabu vya dini vinakataza riba, na kwa kutambua hilo, ZIC Takaful imeanzisha huduma za bima zinazozingatia misingi ya Kiislamu ili kuwawezesha Waislamu na wasiokuwa Waislamu kupata kinga ya bima bila kwenda kinyume na imani zao.

Ameeleza kuwa kwa muda mrefu baadhi ya waumini wamekuwa wakisita kujiunga na huduma za bima kutokana na wasiwasi wa kukiuka misingi ya dini.

Kwa mujibu wa ZIC Takaful, lengo kuu la bima ya Takaful ni kusaidiana wakati wa majanga na changamoto mbalimbali, tofauti na baadhi ya mifumo ya bima ya kawaida inayojikita zaidi katika misingi ya kibiashara.

Sauti ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZIC Takaful, Said Abdallah Sleyum.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi Sleyum amewahimiza viongozi hao kuyatumia mafunzo hayo kuielimisha jamii inayowazunguka kuhusu umuhimu wa kujiunga na huduma za Takaful.

Sauti ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZIC Takaful, Said Abdallah Sleyum.

Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa dini wameahidi kuyatumia mafunzo hayo katika kuelimisha jamii wanazoziongoza ili kuitumia ZIC Takaful, wakieleza kuwa huduma hiyo ina manufaa kwa watu wa dini zote na inaweza kusaidia kuiepusha jamii na mifumo ya riba.

Sauti ya Viongozi wa dini.

Mafunzo hayo kwa viongozi wa dini yamefanyika katika mikoa mitatu ya unguja ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kampuni kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa bima ya Takaful na kuhamasisha matumizi ya huduma za kifedha zinazozingatia misingi ya dini na maadili.