Zenj FM

Uzinduzi wa maduka ya Airtel waongeza chachu ya uchumi Zanzibar

10 February 2026, 2:59 pm

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mohammed Ali Abdalla akizungumza wakati wa uzinduzi wa maduka manne ya Airtel uliofanyika katika nyumba za ZSSF, Mbweni, Wilaya ya Mjini Magharibi B.

Na Mary Julius.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mohammed Ali Abdalla amesema uzinduzi wa maduka mapya ya Airtel Zanzibar ni hatua muhimu katika kusogeza huduma karibu na wananchi pamoja na kufungua fursa zaidi za ajira kwa vijana na wajasiriamali visiwani Zanzibar.

Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa maduka manne ya Airtel uliofanyika katika nyumba za ZSSF, Mbweni, Wilaya ya Mjini Magharibi B.

Ameipongeza Kampuni ya Airtel kwa kuona umuhimu wa kuendelea kufungua maduka zaidi katika visiwa vya Unguja na Pemba, hatua inayoongeza chachu ya uchumi na kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kifedha.

Aidha, amesema sera za uchumi na uwekezaji za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya maono ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, zimeendelea kuunda mazingira rafiki ya uwekezaji, jambo lililowezesha Airtel kufikia mapato ya zaidi ya dola milioni 467, huku idadi ya wateja ikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 17.3 duniani kote.

Mkuu wa Mkoa amewataka wawekezaji kuendelea kushirikiana na serikali, akisisitiza kuwa maduka hayo yatasaidia wananchi kupata huduma za mawasiliano na kifedha bila usumbufu, karibu na maeneo yao.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mohammed Ali Abdalla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Airtel, Adrianna Lyamba, amesema uzinduzi wa maduka hayo manne Zanzibar ni sehemu ya mkakati wa Airtel wa kusogeza huduma kwa wananchi kwa haraka zaidi kupitia mifumo ya kidigitali.

Amesema kila duka lina uwezo wa kuwahudumia zaidi ya wajasiriamali 400, hivyo uwekezaji huo unachochea fursa za kiuchumi, biashara na ajira, hasa kwa vijana.

Lyamba ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano mzuri, akiahidi kuwa Airtel itaendelea kuboresha huduma zake ili wakazi wa Zanzibar, wafanyabiashara na wageni wapate mawasiliano ya uhakika na huduma za kifedha zilizo salama na rahisi kutumia.

Sauti ya Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Airtel, Adrianna Lyamba

Naye Meneja wa Airtel Kanda ya Zanzibar, Nassor Twahiri Lazier, amesema uzinduzi wa maduka hayo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa Zanzibar.

Amewahimiza wananchi wanaoishi karibu na maduka hayo kuyatumia kikamilifu ili kupata huduma bora za Airtel.

Sauti ya Meneja wa Airtel Kanda ya Zanzibar, Nassor Twahiri Lazier.

kampuni ya Airtel imezindua maduka 31 Tanzania nzima na kwa upande wa Zanzibar maduka 4 yameyozinduliwa ambayo yapo katika maeneo ya Nyumba za ZSSF Mbweni,Kwerekwe, Amani na upande wa pemba duka lipo Chakechake.