Zenj FM

Madiwani Manispaa Kati watakiwa kuibua vyanzo vipya vya mapato

7 February 2026, 9:38 pm

Mkuu wa Wilaya ya Kati Ndugu Rajab Ali Rajab wa Kati akisikiliza kwa makini hoja za Madiwa katika kikao cha tathmini ya makadirio, makusanyo na matumizi ya fedha kwa robo ya pili ya Mwaka 2025/2026, kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Manispaa Kati Dunga Wilaya ya Kati Unguja.

Na Hakika Mwinyi Mwaka.

Madiwani wa Baraza la Manispaa Kati wametakiwa kuwa wabunifu katika kuibua vyanzo vipya vya mapato kwa lengo la kuongeza mapato katika Manispaa hiyo.

Hayo ameyasema Mkuu wa Wilaya ya Kati Rajab Ali Rajab katika kikao cha Baraza la Madiwani cha kuwasilisha taarifa ya makadirio, makusanyo na matumizi ya fedha kwa robo ya pili ya mwaka 2025/2026 hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Manispaa Kati Dunga Wilaya ya Kati Unguja.

Amesema iwapo watashirikiana kwa pamoja wataisaidia Manispaa kuongeza mapato kwa haraka kupitia nyanja mbalimbali na kuzitatua changamoto zinazowakabili Wanchi katika Wadi zao .

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kati Rajab Ali Rajab.

Akiwasilisha  taarifa ya makadirio, makusanyo na matumizi ya fedha kwa robo ya pili ya mwaka 2025/2026 Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Kati Daktari Mwanaisha Ali Said amesema kwa upande wa mapato Baraza hilo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa kipindi cha robo ya pili Oktoba hadi Disemba limekadiria kukusanya jumla ya shilingi Milioni 450 na limefanikiwa kukusanya jumla ya Milioni 314 na 5000 sawa na asilimia 69 ya mapato yote.

Sauti ya Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Kati Daktari Mwanaisha Ali Said.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa  Baraza la Manispaa Kati Said Hassan Shaabani amesema katika Kikao hicho mambo mbalimbali yamejadiliwa ikiwemo Miradi ya maendeleo, harakati za Usafi na ukusanyaji wa mapato ili kuhakikisha Baraza hilo linapiga hatua kimaendeleo.

Sauti ya Mstahiki Meya wa  Baraza la Manispaa Kati Said Hassan Shaabani.

Nae Diwani wa kuteuliwa viti maalumu Tendani Mkanga Miraji amewaomba Wananchi kushirikiana na Baraza hilo katika  masuala mazima ya Usafi ili Baraza liweze kufikia malengo katika ukusanyaji wa mapato.

Sauti ya Diwani wa kuteuliwa viti maalumu Tendani Mkanga Miraji.