Zenj FM

Kambi ya tiba na upasuaji yarejesha tabasamu kwa wananchi Kitogani

6 February 2026, 11:17 pm

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji,akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Seifee Hospital Zanzibar, Dkt. Murtaza Haiderbhai, na baadhi ya madaktari na daktari dhamani wa hospital ya Kitogani, mkoa wa Kusini unguja.

Na Mary Julius.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji, ameipongeza Seifee Hospital Zanzibar kwa kuendesha kambi maalum ya tiba na upasuaji, akisema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa moja kwa moja wa malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuboresha huduma za afya na kusogeza madaktari bingwa karibu na wananchi.

Dkt. Miraji ametoa pongezi hizo wakati wa kufunga rasmi kambi ya tiba na upasuaji ya siku tatu iliyofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Kitogani, Mkoa wa Kusini Unguja. Kambi hiyo ilidhaminiwa na Project Rise, mpango wa Jumuiya ya Dawoodi Bohra, kwa kushirikiana na Seifee Hospital Tanzania na Seifee Hospital Zanzibar Limited.

Amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliipa Seifee Hospital dhamana ya kusimamia hospitali za wilaya 10 za Unguja na Pemba, na moja ya masharti muhimu katika makubaliano hayo ilikuwa ni kuhakikisha upatikanaji wa madaktari bingwa kwa wananchi.

Aidha, ameitaka Seifee Hospital kuendelea kuandaa kambi kama hizo mara kwa mara, akisisitiza kuwa zina mchango mkubwa katika kupunguza changamoto za huduma za afya, hususan kwa wananchi wa maeneo ya mbali.

Kwa upande mwingine, Dkt. Miraji amezitaka taasisi nyingine zinazosimamia hospitali Zanzibar kuiga mfano wa Seifee Hospital kwa kutoa huduma bora, zenye ufanisi, na kuhakikisha madaktari bingwa wanapatikana kwa wakati kwa wananchi.

Sauti ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji,Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji,

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Seifee Hospital Zanzibar, Dkt. Murtaza Haiderbhai, amesema Hospitali ya Wilaya ya Kitogani imekuwa kitovu cha matumaini mapya kwa wananchi, ambapo kambi hiyo imetoa huduma za upasuaji wa jumla, upasuaji wa wanawake, mifupa, macho, afya ya uzazi pamoja na uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa wagonjwa kutoka Unguja na Pemba.

Sauti ya Mkurugenzi Mkuu wa Seifee Hospital Zanzibar, Dkt. Murtaza Haiderbhai.

Naye Daktari Dhamana wa Hospitali ya Wilaya ya Kitogani, Dkt. Dalila Mwindadi, amesema zaidi ya wagonjwa 100 wamefanyiwa upasuaji bila malipo, kupitia kambi hiyo iliyohusisha madaktari bingwa kutoka nchi mbalimbali ikiwemo India, China, Nigeria na Tanzania.

Ameongeza kuwa kambi hiyo imekuwa fursa muhimu ya kuongeza ujuzi na uzoefu kwa wahudumu wa afya na madaktari wazawa kupitia kufanya kazi bega kwa bega na madaktari bingwa wa kimataifa.

Sauti ya Daktari Dhamana wa Hospitali ya Wilaya ya Kitogani, Dkt. Dalila Mwindadi.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliopata huduma za upasuaji wameishukuru Seifee Hospital kwa kuwapatia matibabu bure, wakisema huduma hizo zimewarejeshea matumaini mapya ya maisha.

Aidha Wameomba kambi kama hizo ziendelee kufanyika mara kwa mara, wakisisitiza kuwa afya ni msingi wa maisha ya binadamu.

Sauti ya wananchi.

Kambi hiyo ya tiba na upasuaji imeandaliwa na Project Rise, mpango wa Jumuiya ya Dawoodi Bohra,kwa kushirikiana na Seifee Hospital  Tanzania na Seifee Hospital Zanzibar Limited, ambapo zaidi ya madaktari bingwa 20 kutoka nchi mbalimbali walishiriki.