Zenj FM
Zenj FM
4 February 2026, 10:54 pm

Na Mary Julius.
Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Msafiri Marijani, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kambi za matibabu ya bure ili kupima afya zao, hatua itakayosaidia kugundua mapema maradhi yasiyoambukiza na kupunguza athari zake kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Dkt. Marijani ametoa wito huo wakati wa ufunguzi wa kambi ya siku nne ya upimaji wa afya, iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, Wizara ya Afya Zanzibar na Vodacom Tanzania Foundation kambi inayofanyika katika viwanja vya New amani complex.
Amesema kambi hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, kwa lengo la kuwafikia watu wengi zaidi na kuwaondolea vikwazo vya kifedha vinavyowakwamisha kupata huduma za matibabu.
Amebainisha kuwa kwa sasa dunia inashuhudia ongezeko kubwa la maradhi yasiyoambukiza, huku magonjwa ya moyo yakiongoza kwa kusababisha vifo, yakifuatiwa na ugonjwa wa kisukari, hali ambayo imekuwa mzigo mkubwa kwa familia na serikali.
Kwa mujibu wa Dkt. Marijani, kambi hiyo ya siku nne inalenga pia kuwajengea wananchi utamaduni wa kupima afya mara kwa mara, ili kuzuia madhara makubwa yanayotokana na maradhi yasiyoambukiza ambayo mara nyingi hugundulika yakiwa katika hatua za mwisho.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Juliet Magandi, amesema kambi hiyo inafanyika kwa ushirikiano wa karibu kati ya Hospitali ya Muhimbili, Wizara ya Afya Zanzibar na Kampuni ya Vodacom Tanzania.
Dkt. Magandi amesema wamejipanga kuwafikia wananchi zaidi ya elfu sita kwa kutoa huduma za kibingwa bila malipo, akiongeza kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ina zaidi ya miaka 120 tangu kuanzishwa kwake na ina madaktari bingwa wa fani mbalimbali.
Amesema kambi hiyo inalenga pia kujengeana uwezo kati ya madaktari wa Muhimbili na wale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, huku lengo kuu likiwa ni kugundua mapema maradhi yasiyoambukiza ambayo mara nyingi hayana dalili za awali.
Naye Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald, Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wataalamu wa afya pamoja na wadau mbalimbali ili kupanua mpango huo katika maeneo mengine.
Mpango huo ni sehemu ya mchango wa Vodacom Tanzania Foundation katika kuunga mkono Lengo la Maendeleo Endelevu namba 3 (SDG 3) linalolenga kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote na kuimarisha ustawi wa jamii.
Aidha, meneja Sandra amewaomba wakazi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kambi hiyo ya afya, akisisitiza kuwa uchunguzi wa mapema, uelewa na kinga ni nguzo muhimu katika kujenga familia zenye afya njema na jamii imara.
Kwa upande wao, wananchi waliopata huduma wamepongeza zoezi hilo na kuomba liendelezwe zaidi. Zuhura Khamis Nassor amesema amepata vipimo na kukutana na madaktari bingwa, huku akiomba kambi hizo zipelekwe hadi vijijini na mashambani.
Naye Abdalla Pandu amesema kambi hiyo imemsaidia kufahamu hali ya afya yake na kupata matibabu, amezihimiza taasisi na makampuni mengine kuiga mfano wa Vodacom Tanzania.
Kambi hiyo ya siku nne imeanza siku ya Jumanne na inatarajiwa kumalizika siku ya Ijumaa, tarehe 6 mwezi wa pili.