Zenj FM
Zenj FM
30 January 2026, 12:59 pm

Na Mary Julius.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limesema limejipanga kikamilifu kuhakikisha ulinzi na usalama vinaimarishwa kabla, wakati na baada ya mchezo wa kimataifa wa mpira wa miguu wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, CAF.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Madema, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Thadei Mchomvu , amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, limechukua hatua zote muhimu kuhakikisha mchezo huo unafanyika katika mazingira ya amani na usalama.
Mchezo huo utazikutanisha timu ya Young Africans Sports Club (YANGA SC) ya Tanzania dhidi ya Al Ahly SC ya nchini Misri, na unatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kuanzia saa 10:00 jioni.
Kamishna Mchomvu amesema Jeshi la Polisi linatambua kuwa mchezo huo ni mkubwa na una heshima kwa taifa, hivyo halitaruhusu vitendo vyovyote vinavyoweza kuvunja amani au kuhatarisha usalama wa wananchi, mashabiki na wageni watakaohudhuria mchezo huo.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi, wanachama, mashabiki na wapenzi wa mpira wa miguu kufika uwanjani mapema, ili kuepuka msongamano, na kuzingatia maelekezo yote ya usalama.