Zenj FM
Zenj FM
25 January 2026, 2:06 pm

Na Mary Julius.
Mrajisi wa Asasi za Kiraia Zanzibar, Ahmed Khalid Abdulla, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini kwa kiwango kikubwa juhudi zinazofanywa na jumuiya za wasaidizi wa sheria, akibainisha kuwa zimekuwa na mchango muhimu katika kuwasaidia wananchi, hususan wasio na uwezo, kupata haki na ufumbuzi wa changamoto za kisheria.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mtandao wa Jumuiya za Wasaidizi wa Sheria Zanzibar (ZAPONET), uliofanyika katika Ofisi ya Malaria, MwanaKwerekwe Zanzibar, Mrajisi Ahmed Khalid amesema uwepo wa ZAPONET kama mwamvuli wa jumuiya za wasaidizi wa sheria ni fursa muhimu katika kuunganisha jumuiya hizo na serikali pamoja na kuratibu shughuli zao na kusaidia upatikanaji wa rasilimali ufadhili na kuwajengea uwezo wa kitaalamu katika maeneo mbalimbali.
Amezitaka jumuiya hizo kuimarisha ushirikiano kuanzia ngazi ya wilaya hadi mtandao wa ZAPONET, ili kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinawafikia wananchi wengi zaidi na zenye ubora.
Amesema Ofisi ya Mrajisi itaendelea kufanya jitihada za kutafuta wafadhili ili kuziimarisha jumuiya za wasaidizi wa sheria na kuongeza ufanisi wa huduma wanazozitoa kwa jamii.
Aidha, Amesisitiza umuhimu wa wasaidizi hao kutoka nje ya ofisi zao na kwenda moja kwa moja katika jamii, kushirikiana na masheha pamoja na viongozi wa maeneo kuandaa mikutano ya uhamasishaji, ili wananchi wafahamu aina ya msaada wa kisheria unaotolewa.
Ameongeza kuwa ili taasisi yoyote ya kiraia iweze kufikia mafanikio, ni lazima izingatie misingi ya kisheria ikiwemo kufanya mikutano mikuu halali. Amesema kufanyika kwa mkutano mkuu ni kielelezo cha uwajibikaji na utii wa sheria, huku akionya kuwa jumuiya zisizozingatia taratibu hizo hujiweka katika hatari ya kukiuka masharti ya usajili wa asasi za kiraia.
Aidha, ameipongeza Legal Services Facility (LSF) kwa kuendelea kudhamini shughuli za wasaidizi wa sheria Zanzibar.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ZAPONET Nassor Hakim Haji, ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutenga fungu maalum la bajeti kwa ajili ya kusaidia shughuli za wasaidizi wa sheria zanzibar.
Aidha amesema lengo la mkutano huo ni pamoja na kufanya marekebisho ya katiba ya ZAPONET ili iweze kupitishwa na kutumika rasmi katika kuongoza shughuli zake.
Kwa upande wake mwakilishi wa LSF Bakar Hamad amesema kuanzishwa kwa mwamvuli huu wa ZAPONET utasaidia kupaza sauti ya pamoja kwa jumuiya zote za wasaidizi wa sheria Zanzibar na kusema wataendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha wanafikia malengo walio jiwekea.
Mwamvuli wa ZAPONET unawananchama kumi na moja ambazo ni jumuiya za wasaidizi wa sheiria katika wilaya zote za Unguja na Pemba.