Zenj FM

Miradi ya Manispaa Kati yainua uchumi wa wananchi

23 January 2026, 5:52 pm

Madiwani na Watendaji wa Baraza la Manispaa Kati wakitembelea soko la Mboga Mboga Dunga katika ziara maalumu ya kutembelea miradi ya maendeleo na vyanzo vya mapato vilivyopo ndani ya Manispaa Kati Wilaya ya Kati Unguja.

Na Mary Julius.

Wananchi wa Wilaya ya Kati Unguja wametakiwa kutumia kikamilifu fursa zinazopatikana katika Baraza la Manispaa Kati ili kupunguza gharama za maisha na kukuza mapato ya serikali kwa ujumla.

Wito huo umetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa Kati, ambaye pia ni Diwani wa Wadi ya Koani, Said Hassan Shaaban, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo na vyanzo vya mapato vya kimkakati wilayani humo.

Amesema ziara hiyo imelenga kuhakikisha Madiwani wote wa Manispaa Kati wanaifahamu kwa kina miradi ya maendeleo pamoja na vyanzo vya mapato vilivyopo ndani ya Manispaa, hatua itakayowawezesha kupanua wigo wa mawazo na kubuni mbinu bora za kuboresha vitega uchumi kwa ajili ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Sauti ya Mstahiki Meya wa Manispaa Kati, ambaye pia ni Diwani wa Wadi ya Koani, Said Hassan Shaaban.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Kati, Daktari Mwanaisha Ali Said, amesema ziara hiyo iliyohusisha Madiwani kumi na tano pamoja na Watendaji tisa wa Manispaa imekuwa na mafanikio makubwa, kwani imewawezesha Madiwani hao kuona hali halisi ya miradi na vyanzo vya mapato, kutoa maoni na kupendekeza maboresho katika kila hatua.

Aidha amesema hatua hiyo itachangia kuimarika kwa mapato na maendeleo ya Manispaa Kati kwa ujumla.

Sauti ya Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Kati, Daktari Mwanaisha Ali Said.

Nao Madiwani walioshiriki ziara hiyo wamesema watayafanyia kazi mapungufu yote yaliyojitokeza, kuitangaza miradi iliyopo kwa wananchi ili itambulike zaidi na kuifanya Manispaa Kati kupiga hatua za maendeleo.

Sauti ya Madiwani.

Katika ziara hiyo, jumla ya miradi saba ilitembelewa, ikiwemo soko la samaki Unguja Ukuu Kaepwani, soko la samaki Chwaka, soko la Mboga mboga Dunga, soko la mazao ya baharini Kikungwi, maduka ya Kipilipilini Chwaka, kituo cha wajasiriamali Hanyegwa Mchana pamoja na Bustani ya Jamii Jumbi, Wilaya ya Kati Unguja.