Zenj FM

Uhalifu Zanzibar washuka, ajali barabarani zaongezeka

23 January 2026, 4:48 pm

Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Kombo Khamis Kombo akizungumza huko Makao Makuu ya Polisi Zanzibar wakati akitoa taarifa ya hali ya usalama kwa waandishi wa habari.

Na Mary Julius.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, CP Kombo Khamisi Kombo, amesema jumla ya makosa makubwa ya jinai yamepungua kwa asilimia ishirini na nne nukta tatu kwa mwaka 2025.

Akizungumza wakati wa akitoa tathmini ya hali ya usalama Zanzibar kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2025 , Kamishina amesema makosa 2386 yameripotiwa, ikilinganishwa na makosa 3145 mwaka 2024 , sawa na punguzo la makosa 759.

Amesema makosa dhidi ya binadamu yamepungua kutoka makosa 1116 mwaka 2024  hadi makosa 812 mwaka 2025 .

Kwa upande wa mauaji, Kamishina amesema makosa 53 yameripotiwa mwaka elfu mbili ishirini na tano2025  ikilinganishwa na 66 mwaka 2024, sawa na punguzo la asilimia kumi na tisa nukta saba.

Ameeleza kuwa sababu kuu za mauaji hayo ni pamoja na wananchi kujichukulia sheria mkononi, wivu wa kimapenzi pamoja na ugomvi vilabuni.

Akizungumzia makosa ya kubaka, Kamishina amesema yamepungua kutoka makosa 829  mwaka 2024 hadi 657 mwaka 2025.

Hata hivyo, amefafanua kuwa kati ya makosa hayo, mengi yanahusisha vijana waliokubaliana kwa ridhaa, lakini kwa mujibu wa sheria, msichana aliye chini ya umri wa miaka kumi na nane hutambulika kuwa mtoto, hivyo makosa halisi ya kubaka ni 207.

Sauti ya Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Kombo Khamis Kombo.

Kwa upande wa usalama barabarani, Kamishina amesema makosa yameongezeka kutoka 50016  mwaka 2024  hadi 71495  mwaka 2025.

Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuchukua hatua madhubuti pamoja na kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara, huku akiiomba jamii kushirikiana na vyombo vya usalama kupunguza ajali ambazo bado zinaathiri zaidi wanaume, ambao ni nguvu kazi ya taifa.

Sauti ya Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Kombo Khamis Kombo.

Kutokana na ongezeko hilo la ajali za barabarani, Kamishina amesema Jeshi la Polisi limejipanga kuimarisha doria na oparesheni za usalama barabarani, hususan katika maeneo hatarishi na nyakati za usiku.

Amesema sheria za usalama barabarani zitasimamiwa kwa ukali, ikiwemo kudhibiti mwendo kasi, ulevi barabarani, matumizi ya simu wakati wa kuendesha vyombo vya moto pamoja na uzembe wa madereva.

Aidha, Kamishina Kombo amewataka waandishi wa habari kuzingatia uandishi wa kuelimisha jamii badala ya kuripoti ajali pekee, kwa kueleza chanzo cha ajali na namna ya kuziepuka, na kuepuka uandishi unaoweza kuchochea uzembe, huku wakihamasisha uwajibikaji na kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kampeni mbalimbali za usalama barabarani, hususan kwa vijana na waendesha vyombo vya moto.

Sauti ya Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Kombo Khamis Kombo.