Zenj FM

Changamoto wasaidizi wa sheria Zanzibar ZAPONET yasisitiza uandishi wa miradi

18 January 2026, 8:49 pm

Mkurugenzi wa Mtandao wa Jumuiya za Wasaidizi wa Sheria Zanzibar, ZAPONET Zanzibar, Asia Abdulsalam Hussein, akizungumza wakati wa akitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo jumuiya za wasaidizi wa sheria Unguja, yaliyo tolewa na ZAPONET yaliyokufanyika katika Skuli ya Tumekuja Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Unguja.

Na Mary Julius.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Jumuiya za Wasaidizi wa Sheria Zanzibar, ZAPONET Zanzibar, Asia Abdulsalam Hussein, amesema ili jumuiya za wasaidizi wa sheria ziweze kufanya kazi kwa ufanisi, ni lazima zijikite katika uandishi wa miradi na utafutaji wa wafadhili, hatua itakayowawezesha kujiendesha na kutoa huduma bora za kisheria kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuzijengea uwezo jumuiya za wasaidizi wa sheria Unguja, yaliyo tolewa na ZAPONET na kufanyika katika Skuli ya Tumekuja Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Unguja Mkurugenzi Asia amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo washiriki kwa kuwapatia ujuzi na utaalamu wa namna ya kuandika miradi pamoja na mbinu mbalimbali za kuwafikia wafadhili, ili jumuiya zao ziweze kupata ufadhili na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Amesema Jumuiya za wasidizi wa sheria hufanya kazi kwa kujitolea, hali inayozifanya kushindwa kuwafikia wananchi wengi wanaohitaji msaada wa kisheria.

Amesema kuandaa miradi kutaziwezesha jumuiya hizo kupata rasilimali zitakazosaidia kuimarisha utendaji wao na kuwahudumia wananchi wasio na uwezo.

Mkurugenzi Asia ameongeza kuwa wasaidizi wengi wa sheria hawana uelewa wa kutosha wa uandishi wa miradi, jambo linalowakosesha fursa za ufadhili.

Amesisitiza kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa ZAPOnet ni kuhakikisha inawakusanya na kuwajumuisha wadau wote wanaojishughulisha na masuala ya usaidizi wa sheria katika jamii, pamoja na kuwapatia mafunzo ya uendeshaji wa jumuiya na namna ya kuomba ufadhili kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao.

Aidha, amezishauri Jumuiya za wasaidizi wa sheria kuzingatia matakwa ya kisheria kwa kuandaa vikao vya mwisho wa mwaka, ripoti za mwaka na ripoti za fedha, ili kuepuka hatari ya kufutwa au kusimamishwa na Msajili wa Jumuiya.

Sauti ya Mkurugenzi wa Mtandao wa Jumuiya za Wasaidizi wa Sheria Zanzibar, ZAPONET, Asia Abdulsalam Hussein.

Kwa upande wake, Mkuu wa Miradi wa ZAPONET, Alma’s Mohammed, amesema changamoto kubwa inayozikabili jumuiya nyingi ni kushindwa kuandika miradi ya kutosha kwa ajili ya kuomba ufadhili. Amesisitiza umuhimu wa kuelewa misingi ya uandishi wa miradi na kufuata miongozo ya wafadhili ili kuongeza nafasi ya kupata ufadhili.

Sauti ya Mkuu wa Miradi wa ZAPONET, Alma’s Mohammed.

Wakizungumza baada ya mafunzo hayo, baadhi ya viongozi wa jumuiya za wasaidizi wa sheria wamesema mafunzo hayo yamewapa uelewa mpya na wameahidi kuyatumia kwa vitendo kwa kuanzisha miradi itakayowawezesha kuimarisha huduma za kisheria kwa wananchi.

Aidha, wamewaomba viongozi wa wilaya na majimbo kuendelea kuwasaidia ili kuhakikisha jumuiya za wasaidizi wa sheria zinafanya kazi zao kwa ufanisi na kuwafikia wananchi wenye uhitaji wa msaada wa kisheria.

Sauti za Washiriki.

Mafunzo hayo yametolewa kwa Jumuiya za wasaidizi wa sheria za wilaya zote za Unguja na Pemba.