Zenj FM
Zenj FM
8 January 2026, 9:53 am

Na Mary Julius.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohamed amesema Wizara yake imepata mafanikio makubwa katika kipindi kifupi tangu kuundwa kwake baada ya Uchaguzi Mkuu, hususan katika sekta za ujenzi wa barabara pamoja na usafiri wa anga na baharini.
Akizungumza katika kikao cha kwanza cha wizara hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwanja wa Ndege Terminal III, Waziri amesema wizara hiyo ina sekta mbili kuu ambazo ni Sekta ya Ujenzi na Sekta ya Uchukuzi, na kwamba utekelezaji wa miradi katika sekta hizo umeanza kuleta matokeo chanya kwa maendeleo ya Zanzibar.
Waziri ameeleza kwa sasa zaidi ya kilomita 1,084 za barabara zinajengwa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, hatua inayolenga kuboresha miundombinu ya usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Aidha, flyover mpya ya Mwanakwerekwe tayari imekamilika, huku kukamilika kwa flyover ya Amani kukitarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari katika eneo hilo.
Katika sekta ya usafiri wa baharini, Waziri amesema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi ameshaagiza ujenzi wa Bandari ya Tumbatu, ambapo tayari mkandarasi amepatikana na shughuli za ujenzi zinatarajiwa kuanza rasmi hivi karibuni, sambamba na hilo, Bandari ya Mkokotoni inaendelea kuboreshwa kwa kiwango kikubwa ili kuongeza ufanisi wa huduma.
Kwa upande wa usafiri wa anga, Waziri amesema miradi mikubwa inaendelea kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Pemba ambacho kitafungua fursa za kiuchumi na kukuza sekta ya utalii katika kisiwa hicho.
Aidha, Kiwanja cha Ndege cha Nungwi kinatarajiwa kuwawezesha watalii kushuka moja kwa moja katika eneo hilo bila kupitia maeneo mengine.
Akitoa takwimu, Waziri amesema mwezi Disemba 2024 idadi ya abiria waliotumia huduma za uwanja wa ndege ilikuwa 2,010,479, huku mwezi Disemba 2025 idadi hiyo ikifikia 277,177 sawa na ongezeko la asilimia 8.2.