Zenj FM

Rais Samia kuzindua majengo ya kisasa ya sayansi Zanzibar

6 January 2026, 10:19 pm

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Andey Lazaro (katikati) wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa taasisi hiyo iliyopo Buyu wilaya ya Magharib B.

Majengo yatakayozinduliwa  yanajumuisha jengo la taaluma na utawala pamoja na bweni la kisasa la wanafunzi yaliyojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 11 za Kitanzania.

Na Mary Julius.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua jengo la Taaluma na Utawala pamoja na Bweni la wanafunzi katika Taasisi ya Sayansi za Bahari, lililopo Buyu, Wilaya ya Magharibi B, Zanzibar uzinduzi utakaofanyika siku ya tarehe 8 January.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Andey Lazaro, ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa taasisi hiyo.

Amesema uzinduzi huo ni hatua ya kimkakati katika utekelezaji wa ajenda ya serikali ya kuimarisha miundombinu ya elimu ya juu, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Profesa Lazaro ameeleza kuwa ujenzi wa majengo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi, inayosimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.

Amefafanua kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa jengo la taaluma na utawala pamoja na bweni la kisasa la wanafunzi, ambao utasaidia kuongeza uwezo wa taasisi hiyo katika kuhudumia wanafunzi wengi zaidi.

Ameongeza kuwa kupitia mradi huo, Taasisi itaongeza ubora wa utoaji wa programu za elimu kuanzia ngazi ya cheti, shahada za awali hadi shahada za uzamili, kwa lengo la kuzalisha wataalamu watakaohudumia sekta za umma na binafsi, hususan katika nyanja za sayansi ya bahari na maendeleo endelevu.

Aidha, Profesa Lazaro ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwekeza katika elimu ya juu na utafiti kama nguzo ya maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari ya UDSM, Dkt. Mwita Mangora, amesema Taasisi hiyo ni kituo pekee cha elimu ya juu cha chuo kikuu katika masuala ya sayansi ya bahari kwa ukanda wa Afrika Mashariki.