Zenj FM

Wananchi wahamasishwa kushiriki Travelport Fumba Marathon 2026

22 December 2025, 4:00 pm

Mratibu wa mbio za Travelport Fumba Maradhon 2026, Augustine Rutasingwa, akizungumza na vyombo vya habari katika ofisi zake Fumba.

Na Mary Julius.

Katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na maradhi mbalimbali na kuimarisha afya zao, wadau mbalimbali wamejitokeza kuhamasisha jamii kushiriki mashindano ya mbio yanayojulikana kwa jina la Travelport Fumba Marathon.

Akizungumza na vyombo vya habari katika ofisi zake Fumba, Mratibu wa mashindano hayo, Augustine Rutasingwa, amesema mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Februari 14, 2026 katika mitaa ya Fumba, zikilenga kuwashirikisha wananchi wa rika zote hususan jamii inayozunguka eneo hilo.

Amesema kutakuwepo na mbio za familia kwa watoto wenye umri wa miaka 4 hadi 7, zitakazokuwa na umbali wa kilomita moja, pamoja na mbio za watu wazima zenye umbali wa kilomita 5, 10 na 21.1, ambazo zitafanyika kwa mara ya kwanza.

Rutasingwa ameongeza kuwa mashindano hayo yanatarajiwa kuwashirikisha wananchi kutoka maeneo ya Fumba, Nyamanzi, Bweleo, Dimani, pamoja na washiriki kutoka Zanzibar, Tanzania Bara na nje ya nchi.

Sauti ya Mratibu wa mashindano hayo, Augustine Rutssingwa.

Kwa upande wake, Meneja Mauzo wa kampuni ya Travelport Tanzania na Comoro, Jenemiah Mtui, amesema kampuni yao imefarajika kushiriki tukio hilo linalohusisha moja kwa moja jamii, na kuahidi kuendelea kushirikiana na wadau pamoja na serikali katika kutoa huduma bora.

Sauti ya Meneja Mauzo wa kampuni ya Travelport Tanzania na Comoro, Jenemiah Mtui,

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Zanzibar, Muhidini Yassin Masunzu, amesema shirikisho limeshirikishwa kikamilifu katika maandalizi ya mashindano hayo na tayari limetoa kibali rasmi, huku maandalizi ya kiufundi yakiendelea vizuri.

Sauti ya Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Zanzibar, Muhidini Yassin Masunzu

Zawadi mbalimbali zitatolewa, ikiwemo fedha taslimu kwa washindi wa kwanzakatika mbio za kilomita 21, 10 na 5.

Mashindano hayo yamedhaminiwa na Zanziholics Digital Agency, Travelport, Fumba Town, Hospitali ya Ampola Tasakhtaa, Fortitude Total Security (FTS) pamoja na Mixx by Yas.