Zenj FM
Zenj FM
16 December 2025, 9:29 pm

Na Mary Julius.
Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF), Khalifa Hilal Muumin, amewataka Masheha kote Zanzibar kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi katika shehia zao kuhusu Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF), hatua itakayorahisisha zoezi la usajili hususan kwa wanachama wa sekta isiyo rasmi.
Muumin ametoa wito huo wakati akizungumza katika mafunzo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Studio Raha Leo, yaliyolenga kuwajengea uwezo Masheha na wadau mbalimbali ili kusaidia ZHSF kutoa elimu sahihi juu ya huduma na upatikanaji wake kwa jamii inayowazunguka, hasa wakati huu mfuko unapojielekeza katika kusajili wanachama wa sekta isiyo rasmi.
Amesema Masheha wana nafasi kubwa ya kutumia mamlaka na ushawishi wao kuijenga jamii kuelewa umuhimu wa ZHSF, akisisitiza kuwa mfuko huo unasaidia wananchi kuepuka matumizi ya fedha za mfukoni pale changamoto za kiafya zinapojitokeza.
Amefafanua kuwa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar ni mpango maalum wa Serikali uliobuniwa kwa lengo la kuimarisha mfumo wa afya kwa wote na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya wakati wowote bila vikwazo vya kifedha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Programu wa Shirika la Pharma Access, Dkt. Faiza Abbas, amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha dhamira ya afya bora kwa wote inafikiwa.
Akizungumza kuhusu usajili wa sekta isiyo rasmi, Kauthar Ali Suleiman, mmoja wa maofisa hao, amesema kundi kubwa la wananchi lipo katika sekta hiyo, hivyo linahitaji nguvu ya ziada katika uhamasishaji na uelewa ili kufikia malengo ya usajili.
Kwa upande wao, Sheha wa Shehia ya Kwamtumwajeni Rajabu Ali, naSheha wa Shehia ya Fuoni Kipungani, Maltina Rafael Daniel, wameahidi kuongeza juhudi katika kutoa elimu kwa jamii ili wananchi wengi zaidi wajisajili katika mfuko huo.
Aidha, Masheha hao wameishukuru ZHSF na Pharma Access kwa kuwapatia elimu hiyo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha wananchi wote ambao bado hawajasajiliwa wanapata fursa ya kujiunga.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) chini ya udhamini wa Shirika la PharmaAccess.