Zenj FM
Zenj FM
15 December 2025, 4:02 pm

Na Mary Julius.
Mtandao wa Jumuiya za Wasaidizi wa Sheria Zanzibar, ZAPONET, umeanzishwa kwa lengo la kuzijengea uwezo taasisi zinazotoa huduma za msaada wa kisheria Unguja na Pemba ili ziweze kujisimamia na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea Jumuiya za Wasaidizi wa Sheria katika wilaya za Magharibi A, Kaskazini B na Kaskazini A, Mshauri Elekezi wa ZAPONET, Asia A. Hussein, amesema mtandao huo unalenga kuimarisha uwezo wa taasisi hizo kiutendaji, kiuchumi na kitaaluma.
Aidha amesema changamoto zilizokuwa zikizikabili jumuiya hizo zilikuwa nyingi, hivyo ujio wa ZAPONET utasaidia kuhakikisha wanapata msaada wa kutosha na kujengewa uwezo wa kitaasisi ili kufikia malengo yao.
Kwa upande wake, Katibu wa ZAPONET Othuman Abass Othoman amesema lengo la ziara hiyo ni kuitambulisha rasmi ZAPONET kwa jumuiya za wasaidizi wa sheria, kuimarisha mashirikiano na kuhakikisha kila mwanachama anaielewa dhima ya mtandao huo.

Naye Mratibu wa Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Magharibi A, PAUWA Safia B. Amran, amewahimiza wananchi kuzitumia jumuiya za wasaidizi wa sheria ili waweze kupata haki zao kwa urahisi, huku akiomba ushirikiano wa karibu kati ya ZAPONET na jumuiya hizo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini B, NOBPO Shaban Sarboko Makarani amesema ujio wa ZAPONET ni faraja kubwa kwani utaimarisha ubadilishanaji wa uzoefu, maarifa na mbinu za kutatua changamoto mbalimbali, pamoja na kusaidia upatikanaji wa rasilimali fedha.

Ziara ya ZAPONET imehitimishwa Wilaya ya Kaskazini A, ambapo Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini A NAPAC Asia Fadhili Makame amesema kuanzishwa kwa mtandao huo kutapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zinazozikabili jumuiya za wasaidizi wa sheria, huku wakitoa wito wa ushirikiano wa pamoja ili kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwa mwamvuli huo.