Zenj FM
Zenj FM
10 December 2025, 10:50 pm

Na Mary Julius.
Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) upande wa Zanzibar Saleh Haji Pandu amesema serikali imekuwa ikipoteza mapato kutokana na ukosefu wa uelewa katika uuzaji wa rasilimali, hususan kwa wale wanaohusika moja kwa moja na mchakato wa ubadilishaji hati.
Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha wadau kutoka sekta binafsi na serikali, Naibu Kamishna huyo amesema TRA imeamua kutoa mafunzo maalum kwa wanasheria na taasisi za ubadilishaji hati ili kuhakikisha kila muamala wa uuzaji rasilimali unafanyika kwa kufuata taratibu za kodi.
Amesisitiza kuwa kabla ya kubadilisha umiliki wa rasilimali, mnunuzi anatakiwa kuhakikisha muuzaji ameshakamilisha malipo ya kodi na kupata hati safi ya kodi. Hatua hiyo, itasaidia serikali kupata mapato yake kwa uhakika na kuondoa mianya ya upotevu wa kodi.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Jambia Said Jambia, amesema semina hiyo imewasaidia kujifunza zaidi kuhusu sheria ya kodi na malipo ya capital gain.
Jambia amesema matarajio yao ni kwamba watunga sheria wataangalia mazingira ya Zanzibar ili kuondoa mkanganyiko wa sheria na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Naye Wakili wa Mahakama Kuu Zanzibar Neema Alex amesema mafunzo hayo yatawasaidia wanasheria kuwaelimisha wateja wao ili kila mwananchi aweze kulipa kodi ipasavyo.
Ameongeza kuwa changamoto iliyojitokeza ni wananchi wengi wa Zanzibar kudhani kuwa kodi zinazokusanywa na TRA Zanzibar zinapelekwa Muungano, hali ambayo si kweli, kwani kodi hizo zinatumika moja kwa moja Zanzibar.