Zenj FM
Zenj FM
29 November 2025, 10:09 pm

Na Mary Julius.
Uwepo wa treni ya mwendokasi pamoja na maboresho ya viwanja vya ndege katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mikumi umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watalii wanaotembelea hifadhi hiyo.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Kanda ya Mashariki, Fredrick Malisa, amesema kuimarika kwa miundombinu hiyo kumewezesha ongezeko la watalii katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Malisa amesema kuwa katika kipindi hicho, jumla ya watalii 62,468 wametembelea Hifadhi ya Mikumi, ongezeko la asilimia 1.18 ikilinganishwa na matarajio ya watalii 61,742.
Aidha, katika kipindi hicho hifadhi imekusanya jumla ya shilingi bilioni 3.930239203, ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.44.
Ameeleza kuwa hifadhi inaendelea na mkakati wa kuongeza idadi ya watalii kupitia uboreshaji wa miundombinu ya michezo na mikutano, pamoja na kutumia fursa ya treni ya mwendokasi kufungua geti jipya katika maeneo ya Kilosa, litakalojulikana kama Lango la Chamgore.

Katika hatua nyingine, Malisa amesema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya uchimbaji wa visima vitakavyosaidia kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji ndani ya hifadhi.
Afisa Uhifadhi Mwandamizi, Hellen X. Mchaki amesema hifadhi ya Mikumi imekuwa ikinufaika kwa ongezeko la wageni wanaotembelea watalii wengi sasa wanatumia njia mbili kuu ambazo ni kwa njia ya Reli ya mwendokasi, na Usafiri wa anga, ambayo imepunguza gharama na kurahisisha safari, hivyo kuongeza idadi ya wageni .
Nao Walimu na wanafunzi waliotembelea hifadhi hiyo wamesema wamejifunza mambo mengi ambayo awali walikuwa wakiyasoma darasani.
Wamesema Ziara hiyo imewawezesha wanafunzi kuona wanyama kwa macho na kujua maisha yao ndani ya hifadhi.
Aidha Wanafunzi hao Wamewaomba wazazi na walimu wa shule mbalimbali kujitokeza na kuwaleta wanafunzi kutembelea hifadhi hizo ili kuongeza uelewa na kujenga uzalendo.